Serikali imewataka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro na kuwahimiza wapande miti ili kulinda barafu isiyeyuke na hivyo kuendelea kuvutia watalii.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Moshi Mjini, Prof. Patrick Alois Ndakidemi aliyeuliza Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha programu za upandaji miti katika Mlima Kilimanjaro kutokana na kuyeyuka kwa barafu.
Amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeanzisha programu za upandaji miti maeneo ya milima, vilima na miinuko pamoja na kuendelea kutoa elimu ya upandaji wa miti.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Khamis amewahimiza wananchi katika kila kaya kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda ili kuunga mkono jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira kwa ujumla.
Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Asha Abdullah Juma aliyetaka kufahamu Serikali imejipanga vipi kuongeza kasi ya upandaji miti ili kulinda mazingira amesema katika kuongeza kasi ya upandaji miti, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Wizara za kisekta na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na wadau wengine imeendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi na Sekta Binafsi kupitia kampeni ya kitaifa ya upandaji miti millioni 1.5 kwa kila halmashauri nchini.
Amefafanua kuwa mwaka 2023/24 jumla ya miti Milioni 226.97 ilipandwa, kati ya miti hiyo Milioni 211.81 ilistawi sawa na asilimia 76.5. Tathmini ya miti iliyopandwa kupitia kampeni hii kwa mwaka 2024/25 inaendelea.
Amesema Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu mazingira na kuhamasisha wananchi kupanda miti kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo kwa mwaka 2024/25 jumla ya miti milioni 150.16 ilipandwa.
Katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar na miaka 60 ya Muungano, Naibu Waziri Khamis amesema kwa mwaka 2024, miti zaidi ya 53 ilipandwa.
Naibu Waziri Khamis amesema kuwa tathmini ya miti iliyopandwa kupitia utaratibu huu kwa mwaka 2024/25 inaendelea kufanyika na ikikamilika itatolewa kwa umma.
Akiendelea kujibu swali la nyongeza la Asha amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ina maafisa viungo katika kila mkoa ambao wanafuatilia ufanisi wa upandaji miti katika maeneo hayo na kuandaa taarifa.
Ameongeza kuwa kampeni ya ‘Soma na Mti’ ambayo inaelekeza kila mwanafunzi apande mti, inasaidia katika kuongeza wigo wa upandaji wa miti hususan kupitia klabu za mazingira katika shule mbalimbali.