Zaidi ya Wajasilimali 300 kutoka Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani wamepata elimu ya ujasilimali na mafunzo ya utunzaji wa fedha kutoka Taasisi ya CRDB bank Foundation lengo likiwa ni kuliwezesha kundi hilo kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa tija.
Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika leo Ijumaa,February 14,2025 Kibaha Mkoani Pwani ikiwa ni mwendelezo wa Taasisi hiyo juu ya program maalumu ya kutoa mafunzo ya ujasilimali,elimu ya fedha,ubunifu na teknolojia jumuishi pamoja na mitaji ya fedha.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Afisa kutoka CRDB Foundation makao makuu, Husna Ngoda amesema kuwa Taasisi hiyo ilifanya utafiti na kuona kundi la wanawake na vijana limekuwa likifanya shughuli za ujasilimali bila kuwa na elimu ya kutosha jambo ambalo ni hatari kwao.
“CRDB Foundation ni kampuni tanzu ndani ya benk ya CRDB tumejikita zaidi kusaidia kundi la wawake na vijana wajasiliamali tunawapa elimu ya ujasilimali utunzaji wa pesa na hata kuwawezesha mitaji ya biashara zao”amesema.
Amesema kuwa katika kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuiwezesha jamii kimaendelel Taasisi hiyo inashirikiana na mashirika mbalimbali nchini ili kuwafikia wanawake wengi.
“Tangu Taasisi hii ilipoanzishwa mwaka 2023 imeshawafikia wanawake zaidi ya laki tatu kwa kuwapa mafunzo ya ujasiliamali na kuwawezesha mitaji”amesema.
Mwenyekiti wa chama cha wanawake wafanyabiashara nchini kwa ngazi ya Mkoa wa Pwani (TWCC) Stellar Gwassa amesema kuwa changamoto kubwa zinazowakabili wanachama wake ni mitaji na masoko ya uhakika.
Afisa maendeleo ya jamii kutoka Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani Mkaminoela Hangaya amesema kuwa uwepo wa Taasisi zinazojihusisha na kutoa elimu ya ujasilimali kwa wafanyabishara kunasaidia juhudi za kuchochea maendeleo kwa jamii.