Wadau wa elimu Jijini Mwanza, wameipongeza Serikali kwa kutatua changamoto ya miundombinu ya kujifunzia kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Buhongwa.

Akizungumza mara baada ya kutembelea shule hiyo, Afisa Elimu Watu wenye uhitaji Maalumu Awali na Msingi katika Jiji la Mwanza, Zakia Ahmed amesema hapo awali shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mabweni, upungufu wa vyumba vya madarasa, ukosefu wa vifaa wezeshi vya kujifunzia watoto wenye mahitaji maalumu sambamba na ukosefu wa uzio wa shule.

“Hapo mwanzo katika shule hii hatukuwa na bweni hata moja la watu wenye mahitaji maalumu lakini mpaka sasa tumejengewa mabweni mawili yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 160 hali ambayo imepelekea kipindi kifupi tumepokea watoto zaidi ya 100 ambao wanaendelea kupata huduma bure chini ya usimamizi wa walimu na walezi wao,” amesema.

Katika hatua nyingine afisa elimu huyo amesema kwa sasa shule hiyo inakabiliwa  na changamoto ya upungufu wa walimu kutokana na idadi kubwa ya watoto wanaozidi kuletwa na wazazi hivyo ameiomba  Serikali kuona namna ya kuwaongezea idadi ya walimu wa  kufunzisha wanafunzi  wenye uhitaji  maalumu katika Jiji la Mwanza.

“Changamoto tuliyonao ni upungufu wa walimu, wanafunzi ni wengi na kila mwanafunzi ana aina yake ya ulemavu tunahitaji Serikali iendelee kutuletea walimu wapya wanao ajiliwa saizi basi hata Mwanza Jiji tukumbukwe mpaka sasa tuna walimu 8, uhitaji ni walimu zaidi 20 kulingana na aina ya ulemavu wa watoto, tuna wenye usonji huyu anatakiwa mtoto mmoja anakuwa na mwalimu mmoja, lakini kwa upande wa afya ya akili inatakiwa kati ya watoto watano mwalimu anatakiwa mmoja,” amesema.

Akimwakilisha Mwalimu Mkuu  wa shule hiyo, Mwl. Phelister Ndegeulaya ameipongeza Serikali kwa kutoa zaidi ya Sh milioni 486 katika kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule hali inayochochea hali ya ujifunzaji na ufundishaji kwa walimu.

“Naishukuru sana Serikali ya Rais Samia katika mwaka wa fedha 2023/2024 na mwaka huu wa fedha 2024/2025 tumepokea jumla ya Sh milioni 486.3 ambazo  zilikuwa zimeelekezwa katika miundombinu ya mabweni mawili wenye mahitaji maalumu ya wavulana na wasichana ambapo kila bweni linachukua wanafunzi 80,” amesema.

Pia tumejengewa vyumba vya madarasa vinne, vyoo pamoja na uzio wa kuzunguka shule ile kuwaweka wanafunzi salama lakini pia tunaishukuru Serikali kwa mchango mkubwa inao uonyesha katika vifaa wezeshi ambavyo vinatusaidia kufundishia wanafunzi wenye mahitaji maalumu,” amesema Mwalimu Ndegeulaya

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalumu Shule ya Msingi Buhongwa, Sasi Nzololo amesema maboresho ya miundombinu shuleni hapo imepelekea wazazi kuhamasika zaidi kuwapeleka watoto kwani hapo awali walikuwa na wanafunzi 10 lakini hivi sasa wana wanafunzi 192.

“Hapo awali tulikuwa na wanafunzi wachache wasiozidi 10 lakini mpaka sasa hivi tuna wanafunzi 192 jambo ambalo limesababishwa na miundombinu kuboreshwa na Serikali yetu chini ya Rais Samia jambo ambalo sisi tunashukuru sana,” amesema.

Maisha: Kilaza kawa kinara wa darasa, kapata shahada
Rais Samia azungumza na Waziri Mkuu wa Ethiopia