Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) imesikitishwa na tukio la hivi karibuni lililotokea Unguja baada ya Mwanamke mmoja Khadija Shaaban Ali (34) kumshambulia na kumjeruhi mke mwenzake Maimuna Said Suleiman (38), kwa visu.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo mbalimbali vya habari, tukio hilo lilitokea Februari 11, 2025 baada ya Wanawake hao kuwa katika gari moja na mume wao nyumbani kwa mke mdogo huko Chukwani, Mkoa wa Mjini Magharibi baada ya Mume wao kuingia ndani na kuwaacha wake zake hao, ndipo mkasa huo ukatokea.
Taarifa zinadai kuwa, Maimuna alianza kupigwa kwa visu na kupiga makelele ya kuomba msaada lakini mumewe hakuweza kutoka kwa wakati na ndipo aliposhambuliwa na kumsababishia madhara ya kimwili.
TAMWA ZNZ kupitia taarifa yake iliyotolewa hii leo na Mkurugenzi wake, Dkt. Mzuri Issa imeeleza kusikitishwa na kitendo cha mume kuondoka na kuwaacha peke yao bila ya hadhari zozote wakati anajua uhalisia wa tabia zao na inasisitiza uchukuaji wa hatua za kisheria dhidi ya wote waliohusika na kadhia hiyo ili iwe funzo kwa wanaopenda kujichukulia sheria mikononi.
“TAMWA ZNZ, inatoa ushauri kwa Serikali kuangalia uwezo wa wanaume wanaooa wake zaidi ya mmoja kama wana uwezo wa kutosha wa kuwahudumia na kuwalinda wake zao. Pia inatoa wito kwa viongozi wa dini kujenga uelewa kwa jamii, hasa kwa wanaume juu ya wajibu wao wa kusimamia haki, usawa na amani katika familia zao,” ilieleza sehemu ya Taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa rekodi za TAMWA ZNZ, tokea mwaka 2016, matukio 27 ya mauwaji ya wanawake na watoto yameripotiwa (wanawake 22 na watoto watano) na matukio zaidi ya 15 ya vipigo kwa wanawake tokea mwaka 2021, ambapo ni matukio machache yaliyopatiwa hatia za sheria.