Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na mitaji ya Umma (PIC), imepongeza Serikali kwa uwekezaji wenye tija na manufaa kwa maendeleo ya nchi, katika kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za ngozi, Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd.
Akiongea mara baada ya kutembelea kiwanda hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Agustine Holle amesema kuwa kutokana na uwekezaji wenye tija waliouona utaiwezesha serikali kuongeza mapato. Vile vile kiwanda hicho kitaunufaisha mkoa wa Kilimanjaro pamoja na mikoa ya jirani kwa kuboresha mfumo wa maisha na kuongeza kipato kwa wakazi hao.
Amesema, wameridhika na uendeshaji wa Kiwanda hicho ambapo kitakapokamilika kwa asilimia 100 kinakwenda kutoa ajira 3,000 kwa ajira za moja kwa moja na ajira nyingine zisizo za moja kwa moja ni 4,000.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ameihakikishia kamati hiyo kuwa ataendelea kusimamia maono ya Serikali kwa kuufanya uwekezaji huo kuwa endelevu na wenye manufaa ya Watanzania.