Simba kwa sasa ni kama kajipata na licha ya kuachwa pointi nne na watani zao wa jadi wanaokimbizana nao kwenye kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, imesaliwa na mechi moja mkononi huku nyota wao pia wakiwa na rekodi zao za kipekee ikiwamo kiungo wao mshambuliaji, Jean Charles Ahoua.

Ahoua aliyesajiliwa na Wekundu wa Msimbazi akitokea Stella Club d’Adjame ya kwao Ivory Coast amekuwa na msimu mzuri hadi sasa akiwa na mabao manane ana jambo lake huku timu yake ikiwa imesaliwa na michezo 12 kabla ya Ligi Kuu kumalizika.

Ni hivi. Nyota huyo ambaye amekuwa na mchango mkubwa Simba, anaisaka rekodi yake aliyoiweka akiwa na Stella Club d’Adjame msimu uliopita ya kufunga mabao 12 na amebakiza mabao manne tu kuifikia kabla ligi haijaisha.

Ahoua aliyejiunga na Simba Julai 3 mwaka jana akitokea Stella, msimu uliopita aliifungia timu hiyo mabao hayo na kuasisti tisa na kumfanya aibuke Mchezaji Bora wa msimu huo yaani MVP kabla ya kuja nchini na kwa sasa akiwa na Simba ameshafunga mabao manane na asisti tano.

Hiyo ina maana kwamba kwa sasa amesaliwa na mabao manne pamoja na asisti nne vilevile ili kufikia rekodi aliyoiacha Ivory Coast na kama ataongeza zaidi ya idadi ya mabao na asisti hizo nne, bado ataivunja kabisa rekodi hiyo iliyompa tuzo ya MVP wa msimu uliopita.

Ujio wa Ahoua Simba ulimfanya awe nyota watatu waliotoka Ivory Coast akiwa MVP baada ya Stephane Aziz KI msimu wa 2022-2023 na Pacome Zouzoua msimu wa 2023-2024 wote waliopo Yanga wakitokea klabu ya ASEC Mimosas.

Licha ya wengi kutokuwa na imani na mwanzo wa Ahoua, kiasi cha kumjadili ikitokana na ukweli alitua Msimbazi akitajwa kwenda kuziba nafasi ya aliyekuwa kipenzi cha timu hiyo, Clatous Chama aliyepo Yanga kwa sasa, lakini kasi na namba alizonazo hadi sasa zimewaziba wengi midomo.

Ahoua amejizoelea umaarufu mkubwa Msimbazi kutokana na kuibeba timu hiyo iwe katika mahindano ya ndani na hata yale y kimataifa, ikiwa imetinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Nyota huyo aliyezitumikia timu za LYS Sassandra na Sewe Sports kisha kutua Stella zote za Ivory Coast, ana uwezo wa kufunga na kutengeneza mabao, huku akicheza nyuma ya mshambuliaji na wakati mwingine akitokea winga ya kulia au kushoto.

Tangu atue Msimbazi, tayari Ahoua ameivunja rekodi ya mabao ya Chama aliyoiweka msimu wa kwanza wa 2018-2019 akitokea Lusaka Dynamos ya kwao Zambia, alipofunga mabao saba na kuchangia mengine asisti tisa za Ligi.

Kwa sasa Ahoua amebakisha ‘asisti’ nne tu kuifikia rekodi ya Chama ya msimu wa kwanza japo ikiwa atafikisha tano ataivuka, japo anatakiwa kuendelea kuonyesha kiwango bora kama alivyofanya ‘Mwamba wa Lusaka’ akiichezea Simba uikiwamo ya kuasisti 15 rekodi ambayo hadi sasa haijavunjwa.

Ujumbe wa Rodri unarejesha matumaini kwa Man City
Manchester United wanamtaka kila mchezaji sokoni