Vigogo wajuu wa CHADEMA inasemekana wanapanga kumfukuza uanachama Lembrus Mchome, kada aliyehoji uteuzi wa Viongozi wa sekretarieti na wajumbe wa kamati kuu.
Vigogo hao pia inasemekana wamedhamiria kumfukuza uanachama kada huyo maarufu na kumvua wadhifa wake wa uenyekiti wa wilaya ya Mwanga, kwa hatua hiyo ya kuhoji uteuzi ambayo imezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii na kuwagawa baadhi ya makada wa Chadema.
Ingawa bado haijajulikana rasmi ni lini, lakini taratibu za kuanda kikao cha mpango kabambe kwa ajili ya kumshughulikia Mchome zimeshakamilika, kinachosubiriwa ni wahusika kuketi kwa ajili ya ajenda moja ya kumfukuza.
Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa endapo Mchome atafukuzwa uanachama baadhi ya makada waandamizi wakiwemo wajumbe wa baraza kuu wanahisia kutokukubaliana na uonevu huo na kwamba watamsapoti kwa hatua atakazochukua.
“Hatutakubali kwa sababu hajafanya kosa lolote kwa hatua yake ya kuhoji. Sasa ikitokea amefukuzwa tutakuwa naye bega kwa bega hata akienda mahakamani kudai haki yake.
“Tunajua Mchome hayuko vizuri na (mjumbe wa kamati kuu) pamoja na (Naibu katibu mkuu Bara) ambao walitofautiana wakiwa viongozi wa kanda ya Kaskazini. Tunajua watatumia fursa hii kumshughulikia Lembrus,” alisema mmoja wa makada.
Inaarifiwa kuwa hivi sasa bado hakujatulia ndani ya Chadema kuna mpasuko wa viongozi na wanachama na hakuna umoja na kwamba suala la Mchome likitokea litatochechea hali kutokuwa nzuri.
Barua iliyosambaa mtandaoni jana iliyoandikwa na Mchome kwenda kwa katibu mkuu Mnyika amehoji uhalali wajumbe wa kamati kuu na sekretarieti kuthibitishwa na Baraza Kuu la Chadema lililoketi Januari 22 pasipo akidi kutimia.
Inasemekana tangu kumalizika uchaguzi kumekuwa na kutunishiana misuli baina pande mbili zinazomuunga mkono Lissu na Mbowe na suala linalowapa wakati mgumu Chadema ni la No Reforms No election ambayo miongoni mwao hawaielewi kabisa na kubaki njia panda.