Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake Nchini, Mary Chatanda amewataka Wanawake wote waliochaguliwa na kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika 2024 kuwahudumia Wananchi bila ubaguzi.

Chatanda ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na Viongozi hao katika kikao maalum cha mafunzo ya uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, na kusema nafasi walizozipata wanapaswa kuzigeuza kuwa kimbilio kwa watu wote.

Amesema, “nafasi uliyopewa na Wananchi unatakiwa kuitumia kuwanufaisha bila kujali huyo mwananchi ametokea katika chama gani kwa sababu maendeleo ya sehemu Fulani haya angalii anayeishi hapa ana itikadi gani na pale unapofanya vizuri wananchi watakukimbilia tu kueleza shida zao toeni suluhu ya matatizo yao.”

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Benedict Mugambi amesema jukumu la kila kiongozi aliyechaguliwa ni kufuatilia na kujua namna ya kutumia takwimu hizo ili waweze kujenga hoja za kimaendeleo na kuwanufaisha wananchi

Baadhi ya viongozi waliohudhuria semina hiyo wamesema kuwa maafunzo hayo yatawasaidia katika maeneo yao ya kiutawala kwani uongozi unatofautiana kwa kila kiongozi kutokana na namna ya uchaguzi unavyokuwa

Semina hiyo, iliyoandaliwa na ofisi ya takwimu Taifa imehusisha Viongozi wanawake 109 kutoka katika Wilaya za Maswa, Busega, Bariadi, Itilima na Meatu.

Maisha: Dawa ya kuondoa migogoro mikubwa ndani ya ndoa
Mwanza: Polisi wadhibiti mandamano ya CHADEMA