Mkazi wa kijiji cha Burungu kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mkoani Mara, Herman Juma (45) anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake na kutokomea naye kusikojulikana.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, amesema mtu huyo alichukuliwa Februari 14, 2025 na watu waliojitambulisha kuwa ni maafisa usalama wakiwa na gari la kiraia na kisha kuondoka naye.

Amesema, ”Watu hao wakiwa na gari la kiraia waliondoka na mtu huyo na hadi sasa hajulikani aliplekwa kituo gani,kutokana na taarifa hiyo Jeshi la Polisi mkoa wa Mara lilianza uchunguzi mara moja ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo lakini pia kubaini chanzo cha tukio hilo.”
Naye Mke wa mtu huyo, Pendo Turutumba ameesema mumewe hakuwa na uhasama na mtu yeyote hapo kijiji kwao huku akiomba Jeshi la Polisi kusaidia kupatikana kwa mumewe.
Amesema, “siku hiyo nilimuaga mume wangu kuwa nakwenda kutafutia maisha watoto wangu muda si mrefu akanifuata mtoto akaniambia mama unaitwa, ndio nikaenda mpaka kwa Mwenyekiti wa kitongoji akaniambia hao watu wamekuja wakasema wao ni usalama wa Taifa,inamaanisha wenyewe ni maaskari.”
Awali, Mwenyekiti wa kitoji cha Burungu Senta, Matibabu Mbogora alisema aliwaona watu hao ambao walimwamuru kumpigia simu Afisa mtendaji wa kijiji cha Bukumi na alipofika alifanya nao mahojiano na baadaye hakujua kilichoendelea mpaka pale walipoamua kuondoka.
Kufuatia tukio hilo, baadhi ya wakazi wa Kitongoji cha Burungu Senta na Kijiji cha Bukumi wamesema eneo lao halima matukio ya namna hiyohuku wakiomba msaada wa kufanikisha kupatika kwa mwanakijiji mwenzo akiwa salama.