Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Kampuni zinazohusika na Usambazaji wa Mitungi ya Gesi (LPG) -TZLPG kwa lengo la kuwashukuru kwa mchango wao katika utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia  pamoja na kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo utatuzi wa  changamoto zinazoikumba TZLPGA, ili kuhakikisha wanatoa huduma kwa urahisi nchi nzima.

Mazungumzo hayo yamefanyika Februari 20, 2025 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba pamoja Watendaji kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA).

Amesema, “ ili Serikali ifanikiwe lazima kuwashirikisha watu wake, tunawashukuru sana kwa mchango wenu katika kufanikisha Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ambao kutoka tuuzindue mwaka 2024, uelewa na matumizi ya mitungi ya gesi umeendelea kuongezeka, mitungi hii ni gharama lakini ninyi mnajitoa na kutuunga mkono.”

Hata hivyo, Dkt. Biteko amezitaka kampuni hizo kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa mitungi ya gesi  inafika kwa wingi hadi ngazi ya vijiji, ili kuweza kufikia lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 75 ya Wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2030 ikiwa pia ni utekelezaji wa Mpango wa Mahsusi wa Nishati ( Energy Compact uliosainiwa mwezi Januari 2025.

Amesema, lengo la kikao hicho pia lilikuwa ni kujadili changamoto ambazo kampuni hizo wanakutana nazo ikiwemo za kikodi ambazo zina nafasi ya kujadiliwa  katika Muswada wa Masuala ya Fedha utakaosomwa katika Bunge la Bajeti la mwaka 2025/2026.

“Tumekutana hapa ili tunapoelekea kwenye Bajeti ya Serikali mtuambie kipi tukiboreshe kupitia  Muswada wa Masuala Fedha  na ni vizuri pia mkatueleza  jambo gani lifanyike, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa Wananchi,” ameeleza Dkt. Biteko.

Maisha: Mbinu ya kumpata mpenzi wa ndoto zako
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Februari 21, 2025