Katika kutekeleza maagizo wa waziri mkuu ya kuhakikisha uwanja wa ndege wa Shinyanga unaanza kutumika ifikapo mwezi April Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ametembelea kukagua ujenzi wa upanuzi uwanja huo ili kusimamia maagizo ambayo yalitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,kuwa uwanja huo hadi kufikia Aprili ufungwe Taa, na ndege zianze kutua nyakati za usiku.
Katika ziara hiyo Mbarawa amezungumza na wasimamizi wa ujenzi wa Uwanja huo wa Ndege, Wakandarasi,pamoja na kutembelea kuona ujenzi wa miundombinu ya uwanja huo pamoja na kufahamu maandalizi mahususi ya ufaungaji wa taa katika uwanja huo
Amesema ujenzi wa uwanja huo wa ndege pamoja na baadhi ya miundombinu ambayo ni ya muhimu tayari imekamilika, ikiwamo barabara ya kutua na kuruka ndege (Runway),na kuwaagiza wasimamizi wa ujenzi wa uwanja huo na TANROADS, kuhakikisha wanamsimamia Mkandarasi aagize malighafi na kuzifunga Taa kwenye uwanja huo ili kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Majaliwa.
“Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Februari 16 alipofika kwenye ujenzi wa uwanja wa Ndege Shinyanga, aliagiza ifikapo April Mosi, uwanja huu uwekewe Taa, ili uanze kutumika nyakati za usiku, hivyo TANROADS hakikisheni Mkandarasi anaweka “Order ya Material”ili Taa hizo zifungwe na kutekelezwa kwa agizo la Waziri Mkuu,”amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, amempongeza pia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha jitihada zake za kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo wa ndege unafanikiwa pamoja na viwanja vingine vitatu kikiwamo cha Sumbawaga,Tabora na Kigoma,na kwamba haikuwa kazi rahisi, lakini sasa hivi viwanja hivyo vina kwenda kukamilika na kutoa huduma ya usafiri wa Anga kwa wananchi.
Mbarawa amewapongeza pia Wakandarasi kwa uvumilivu wao, kwamba ujenzi wa upanuzi wa uwanja huo wa Ndege Shinyanga ulisainiwa mwaka 2017, lakini katikati ukasuasua, ndipo Rais Samia akasimama kidete ili ujengwe, na ujenzi wake Rasmi ukaanza mwaka 2023, na mpaka sasa wameendelea nao na wapo hatua za mwisho kuukamilisha.
Naye mwakilishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)Lugano Mwinuka, amesema uwanja huo wa Ndege wa Shinyanga, zitakuwa zikitua ndege za masafa ya karibu zenye uwezo wa kubeba abiria 70-76 pamoja na kutumika kama dharura na utakuwa”feeder airport”.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amemshukuru Rais Samia juu ya ujenzi wa uwanja huo wa Ndege, kwamba amefungua fursa za kiuchumi mkoani humo.
Lakini pia Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Donatus Binamungu, amesema ujenzi wa upanuzi wa uwanja huo wa ndege Shinyanga umefikia asilimia 74, na kwamba barabara ya kutua ndege imekamilika kwa asilimia 100 na ndege zinaweza kutua mchana, na kueleza watamsimamia Mkandarasi kuagiza Taa ili zifungwe na kuanza kutumika nyakati za usiku hadi ifikapo mwezi Aprili.