Swaum Katambo – Katavi.
Wanawake mkoani Katavi wametakiwa kuchangamkia fursa adhimu ya kuungana, kusherehekea mafanikio yao na kujiwekea mikakati itakayowawezesha kufikia malengo yao kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwa Mkoa wa Katavi ambayo yanatarajiwa kufanyika Machi 5, 2025 katika viwanja vya shule ya msingi Kashaulili iliyopo Manispaa ya Mpanda na mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa huo Mwanamvua Mrindoko.
Amesema maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha, kuelimisha, na kuchukua hatua za pamoja katika kuleta usawa wa kijinsia, haki, na uwezeshaji wa wanawake kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
“Shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika, zikiwemo bonanza la michezo litakalohusisha mchezo wa netiboli kati ya timu ya wanawake wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na timu ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele” amesema Buswelu
Amesema pia kutakuwa na jukwaa la wanawake kupitia vyombo vya habari, ziara ya kutembelea miradi ya wajasiriamali wadogo, pamoja na kuwatembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Aidha, kutakuwa na ‘usiku wa mwanamke’, tukio maalum la kusherehekea mafanikio ya wanawake na kubadilishana mawazo kuhusu maendeleo yao.
“Wananchi wote wa Mkoa wa Katavi, wadau wa maendeleo, taasisi za umma na binafsi, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, wazee maarufu, wajasiriamali, na wanawake kwa ujumla wanakaribishwa kushiriki kwa wingi katika maadhimisho haya muhimu,” ameongeza.
Maandalizi ya maadhimisho hayo yamefanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha yanafanyika kwa mafanikio makubwa.