Suala la uwezeshaji wa Wanawake wanaoishi katika mazingira magumu na walio Vijijini hasa wale waliotelekezwa na Waume na Familia zao limeendelea kuwa changamoto inayowakabili Wanawake Mkoani Geita, ambapo baadhi yao wamesema uwezeshwaji kwa Mwanamke umewasaidia kujiinua kiuchumi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wanawake hao wameelezea baadhi ya changamoto hizo ikiwemo kukosekana kwa usawa baina ya jinsia ya kiume na jinsia ya kike katika shughuli za maendeleo na fursa kandamizi zinazombana Mwanamke kujiendeleza kiuchumi.

Mmoja wao ambaye ni mkazi wa Shilabela katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Loveness Lema amesema changamoto zimekuwa haziwapi nafasi sawa na Jinsia ya Kiume, huku akishauri kuwepo na mfumo na taratibu za kiserikali zitakazomtambua Mwanamke kama mhitaji wa kuwezeshwa hususani katika Masuala ya Mikopo, Ajira na kufungua fursa nyingi zitakazowapa nafasi katika jamii.
Kwa upande wake, Zaituni Ally na Neema Chodo ambao wote ni Wakazi wa eneo la Mbugani Geita ameeleza kuwepo kwa fursa zinazomtambua Mwanamke ambazo zimesaidia kupunguza matendo yasiyofaa ndani ya jamii ikiwemo Wanawake kujiingiza katika Vitendo vya ukahaba ambapo ameongelea changamoto za Wanawake kuzalishwa na kutelekezwa ambazo zimerudisha nyuma juhudi za Mwanamke kupambana.