Wanafunzi wa Shule ya Msingi Zinga, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, wamesema ni wakati muafaka kwa Serikali kuongeza juhudi katika kuwekeza katika somo la michezo kuanzia elimu ya msingi.

Wanafunzi hao wamesisitiza kuwa uwekezaji huu utasaidia kuibua vipaji vya michezo na kuwawezesha kupata wanamichezo bora watakaoiwakilisha Tanzania kimataifa katika miaka ijayo.

Akizungumza leo Machi 3,2025 baada ya kupokea msaada wa fedha kutoka kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Zinga Mjema.Kashingo wanafunzi hao wamesema kuwa michezo ni fursa muhimu ya kukuza vipaji na uchumi wa taifa, kwani wachezaji wanaweza kujiingizia kipato kupitia michezo na hata kujiajiri katika sekta hiyo.

“Serikali inapaswa kuwekeza zaidi katika vifaa vya michezo na kutoa mafunzo ya kutosha kwa wanafunzi. Tupo wapenzi wa michezo na kuna vijana wengi wenye vipaji. Ikiwa tutawezeshwa ipasavyo, tunaweza kuwa wachezaji bora, na hata kusaidia taifa kujiinua kiuchumi,” amesema mmoja wa wanafunzi hao

Wanafunzi hao wameleza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kukuza afya, kupambana na magonjwa na kuimarisha umoja miongoni mwao.

Kwa kutumia michezo, wanafunzi wanapata nafasi ya kujenga urafiki na kushirikiana, jambo linalosaidia kupunguza vitendo vya ukatili na migogoro miongoni mwao.

“Michezo inawaweka pamoja wanafunzi, inawafanya kuwa kitu kimoja hii ni njia mojawapo ya kupunguza vitendo vya ukatili na kuimarisha upendo,” amesema mwanafunzi mwingine.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Michezo katika shule hiyo, Fakii Mohamedi, amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kwani shule inaelekea kwenye msimu wa mashindano ya Umitashumta yayotarajia kufanyika mwezi Mei mwaka huu.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Zinga, , alikabidhi msaada huo amesema kuwa anaamini kuwa utasaidia wanafunzi katika kukuza vipaji vya michezo.

“Michezo ni afya, lakini pia ni ajira huu ni mwanzo tu na nitashirikiana na wadau wengine kuendeleza juhudi hizi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Polisi wa Kata ya Zinga, Mwajuma Msofe, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi na walimu katika kukabiliana na vitendo vya ukatili miongoni mwa wanafunzi.

“Ushirikiano kati ya mzazi na mwalimu ni muhimu. Mzazi anapaswa kutoa taarifa pindi anapogundua dalili yoyote ya ukatili kwa mtoto wake. Vilevile, wanafunzi wanapaswa kutoa taarifa mara moja kama wanakutana na vitendo vya ukatili ili hatua zichukuliwe,” amesema.

Rais Samia awaandalia Futari Watoto yatima, wenye mahitaji maalum
Afya Tip: Kutokula, kufunga kunarefusha Maisha