Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga leo Machi 4, 2025 ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua kupitia paa la jengo katika Shule ya Sekondari Malimbika, wilayani Gairo, mkoa wa Morogoro.
Akizungumza katika hafla hiyo, Sendiga amewapongeza watumishi wanawake wa Wizara ya Maji kwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa nguvu kazi na rasilimali fedha ili kuwezesha utekelezaji wa mradi hiyo inayolenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na Salama Nchini.
Aidha, Sendiga amesema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 2 katika miradi ya sekta ya maji, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa maji nchini kutoka wastani wa 84% mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.
Akihitimisha hotuba yake, Sendiga amewahimiza wananchi kujenga miundombinu ya kuvuna maji ya mvua katika makazi yao kwa matumizi ya kila siku na kutoa wito kwa wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali ili kufanikisha miradi kama hiyo katika maeneo mengine nchini.
Hafla hiyo, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Ramadhan, wabunge wanawake wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, viongozi wa Chama cha Mapinduzi, watendaji wa Wizara ya Maji, pamoja na wanawake wa mjini Gairo.