Asila Twaha. OR – TAMISEMI.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Rogatus Mativila amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI ambao ni wajumbe wa baraza la wafanyakazi kufanyakazi kwa bidi ili kuendana na kasi ya Serikali.
Ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa ofisi ya Rais – TAMISEMI kilichofanyika jijini Dodoma, chenye lengo la kutoa fursa kwa watumishi kupitia wajumbe wao kujadiliana juu ya masuala mbalimbali yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na maslahi yao.
“Baraza la wafanyakazi linaongeza ushiriki wa wafanyakazi katika uendeshaji wa shughuli za Taasisi kama ilivyofafanuliwa katika sheria ya majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma Sura 105,” amesema Mativila.

Amewataka watumishi kutumia baraza la wafanyakazi kujadili malengo na mipango ya Taasisi ikiwa ni pamoja na maslahi ya watumishi pia amewasisitiza kuwa, mabaraza ya wafanyakazi yanatakiwa kujadili utendaji kazi wa kila siku na jinsi ya kuboresha utendaji kazi zaidi.
Aidha, amewasisitiza wajumbe hao kuhakikisha baraza la wafanya kazi linatakiwa kuwa na wajibu wa kuhakikisha kunakuwepo na maelewano, ushirikiano na mshikamano kati ya wafanyakazi na uongozi wa Taasisi na vilevile linatakiwa kuhakikisha kunakuwepo na nidhamu ya kazi kwa lengo la kuleta tija na ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za Taasisi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Emma Lyimo amemueleza Katibu Mkuu kuwa, kikao hicho ambapo wajumbe ni wawakilishi wa watumishi wengine watapata nafasi ya kuuliza maswali na changamoto zinazowakabili katika majukumu yao ya kazi na pia hupatiwa ufafanuzi hapo hapo sababu kunakuwepo na wakuu wa Idara na Vitengo husika.
“Nitoe rai kwa wakuu wa Idara na Vitengo kushiriki vikao vya baraza la wafanya kazi ambavyo ni muhimu sana sababu ni sehemu ya watumishi kuuliza maswali na kupata majibu” amesema Lyimo
Kikao cha baraza la Wafanyakazi kwa watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Taasisi zake kitakuwa ni cha siku mbili ambapo pia watumishi watapata fursa ya kufundishwa mada mbalimbali ili kujengewa uwezo wa utendaji wa majukumu yao na maisha.