Swaum Katambo, Mpanda – Katavi.

Baadhi ya wanawake mkoani Katavi wamelalamikia changamoto ya kutopata uhuru wa kushiriki katika shughuli za maendeleo na ujasiliamali inayosababishwa na katazo kutoka kwa waume zao na kupelekea kutofanya shughuli zilizokusudiwa pindi wanapopewa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la kiuchumi la wanawake Mkoa wa Katavi Getruda Kilimanjaro wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Shule ya Msingi Kashaulili iliyopo Manispaa ya Mpanda na kusema kuwa hali hiyo inapelekea wanawake hao kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha wamelalamikia uwepo wa changamoto ya kutopata haki za msingi hasa maeneo ya kazi hali inayopelekea rushwa ya ngono licha ya matukio ya namna hiyo kutoripotiwa katika vyombo vya dola.

“Sambamba na hilo waajiri wamekuwa wakiwanyima muda wa kunyonyesha watoto wao wakati wa muda wa kazi baada ya kumaliza muda wa uzazi (maternity leave)” ameongeza.

Kadhalika, wanawake hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutofahamu sheria na haki zao ikiwemo sheria ya kumiliki mali, sheria ya mirathi na ndoa hivyo kujikuta katika wakati mgumu pindi wanapokutana na changamoto zinazolenga maeneo hao.

Akitoa taarifa ya hali ya ukatili wa wanawake katika mkoa huo Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Katavi Kenedy Wilson amesema kwa kipindi cha mwaka 2024 kulikuwa na jumla ya matukio 3,679 ya ukatili dhidi ya wanawake yaliyotolewa taarifa, ambapo kati ya hayo waliopata ukatili wa kimwili ni 1,458,ukatili wa kingono 207,ukatili wa kihisia 1,934 na watoto wa kike waliotelekezwa walikuwa 80.

“Tunaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu juu ya athari za ukatili wa kijinsia na kuchukua hatua kwa wanaobainika ili kusimamia haki stahiki kwa wahanga” Amesema

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Charles Makongoro ambaye amekaimu nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, amesema katika suala la kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kupunguza umasikini ngazi ya familia wanawake kupitia Halmashauri za mkoa huo wameweza kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali,uendeshaji wa miradi na kupatiwa mikopo kwa ajili ya kuboresha miradi yao.

Amewaomba wanawake wa Mkoa wa Katavi kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri lengo likiwa kujikwamua kiuchumi pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali za uongozi zitakazojitokeza kuelekea katika uchaguzi ujao ili kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii na Taifa kwa ujumla.

TANZIA: Prof. Philemon Sarungi ametangulia
Dkt. Mpango ataka Afrika ibuni njia bora uendelezaji rasilimali za Nishati kukidhi mahitaji