Swaum Katambo, Katavi.

Shirika la Umeme Nchini TANESCO Mkoa wa Katavi, limeombwa kutotoa ahadi za lini umeme wa Gridi ya Taifa utawashwa Mkoani hapo, licha ya mradi huo kuonekana kusuasua na kutowashwa kipindi tajwa, hali inayopelekea kutotelekelezeka kwa ahadi hizo.

Hayo yamesemwa katika Kikao cha 24 cha kamati ya ushauri Mkoa wa Katavi (RCC) ambapo baadhi ya wanakamati wakiwemo Madiwani wamedai kuwa kupitia ahadi wanazizipata kutoka kwa Shirika hilo wamekuwa wakizifikisha kwa wananchi na pindi wanapohojiwa juu ya ahadi hizo kutotekelezeka huonekana ni waongo.

“Nakumbuka kikao cha mwisho cha Halmashauri kuu ya mkoa nilihoji,na waliahidi kwamba mwezi wa pili umeme utakuwa umewaka Inyonga lakini hapa (Mpanda) wakaahidi mwezi wa nne umeme itakuwa umefika, sasa mpaka leo mwezi wa tatu umeme Inyonga haujawaka, sasa kwanini tuwe tunaahidi vitu ambavyo tunajua kabisa havitekelezeki?,” amehoji Haidary Sumry Meya wa Manispaa ya Mpanda.

Aidha Sumry amesema anafahamu kuwa ziko jitihada za Serikali kuleta umeme katika mkoa wa Katavi lakini amewashauri Shirika la umeme kama wanaona kuna kusuasua kutotoa ahadi kwa viongozi hao.

“Ahadi tunazopewa tunazichukua na kwenda kuzisema kwa wananchi wetu kwa sababu nimemsikia Tanesco amesema utafika mpanda mwezi wa nne, lakini usipofika mwezi wa nne nikienda tena kwa wananchi mwezi wa tano wananchi si wataniambia mimi muongo?,” ameongeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmshauri ya Mpimbwe, Silas Ilumba amesema, Mkoa wa Katavi unategemea sana upatikanaji wa umeme wa uhakika wa Gridi ya Taifa kwa kuwa unatumia umeme wa jenereta ambao unakata mara kwa mara jambo linalokwisha shughuli za maendeleo.

Naye Mbunge wa Viti maalum Mkoani Katavi, Martha Maliki alihoji ni changamoto gani inayopelekea umeme huo kusuasua na kutowashwa kwa wakati huku akihofia ni namna gani atakwenda kuzungumza na wananchi katika uchaguzi ujao.

Akitolea ufafanuzi hoja hizo mwakilishi kutoka Tanesco Mkoa wa Katavi Mhandisi Godfrey Josephat amesema licha ya ahadi nyingi walizozitoa kwa Serikali na wananchi lakini bado wanaendelea na juhudi mbalimbali kutatua changamoto zilizojitokeza na kuahidi kuja kuzielezea changamoto hizo.

“Sisi kama mkoa tunafanya kazi na msimamizi wa mradi huu pamoja na mkandarasi lakini mpaka naingia kwenye kikao hiki bado sijapata majibu ya lini umeme utawashwa, wananiambia mwishoni mwa wiki hii watanipa majibu ni lini umeme utawashwa,” amesema mhandisi Godfrey

“Mheshimiwa mbunge, kuna mambo mengi ambayo siwezi kuyasema hapa, mkoa kama mkoa Tanesco hatusimamii kabisa huu mradi mkandarasi na msimamizi watakaa mwishoni mwa wiki hii watakuja na taarifa ambayo itakuwa inaonesha ni changamoto zipi ambazo zimetokea mpaka mradi umeshindwa kuwashwa katika mkoa wa Katavi,” ameongeza.

Wabunge Massay, Regina wawagusa Wazazi Manyara
RC Macha awataka Wanawake kujiinua kiuchumi