Watu wawili wamethibitika kuwa na ugonjwa wa Mpox nchini, baada ya Wizara ya Afya kutoa taarifa ya uchunguzi wa maabara uliofanyika kupitia mifumo yake ya ukusanyaji wa taarifa na ufuatiliaji wa magonjwa mara walipopokea taarifa za wahisiwa wenye dalili za ugonjwa huo.

Taarifa iliyotolewa hii leo Machi 10, 2025 na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama imeeleza kuwa dalili za Wahisiwa za kutoka vipele usoni, mikonoji na maeneo mbalimbali ya mwili, ziliambatana na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo ambapo kati ya Wahisiwa hao mmoja ni Dereva wa magari ya mizigo, aliyetoka nchi jirani.

“Baada ya kupokea taarifa za wahisiwa, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa Maabara ya Taifa kwa uchunguzi, March 9, 2025 uchunguzi wa kimaabara
umethibitisha kuwa Wahisiwa wawili wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox,”

“Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na vituo vyote vya kutolea huduma za Afya, inaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna Wahisiwa wengine ili waweze kupatiwa huduma stahiki,” ilieleza semeu ya taarifa hiyo.

Chanzo cha ugonjwa huo ni wanyama jamii ya nyani, ambapo binadamu huweza kuupata kutokana na shughuli zinazoweza kusababisha kugusana na wanyama, majimaji au nyama za wanyama wenye maambukizi na endapo binadamu akipata maambukizi hayo anaweza kumwambukiza mwingine kwa kugusana.

“Kwa taarifa hii, Wizara ya Afya, inawahakikishia Wananchi kuwa Serikali imejipanga kudhibiti ugonjwa huu na hasa kutokana na uzoefu tulionao wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko, Serikali inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote.

PPRA yawanoa Wakaguzi wa ndani matumizi ya NeST
Biashara ya kuuziana umeme kuinufaisha Tanzania - Mha. Mramba