Swaum Katambo, Kavuu.

Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda amezindua kambi ya wiki mbili ya matibabu bure ya macho na matatizo ya mkojo kwa wananchi wa Jimbo hilo lililopo mkoani Katavi.

Hafla ya Uzinduzi huo imefanyika tarehe 11 Machi 2025 katika hospitali ya Wilaya ya Mpimbwe iliyopo Kata ya Tupindo ambapo Pinda amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma ili kuimarisha afya zao na kuendelea na shughuli za uzalishaji.

Kadhalika Pinda amesema ataendelea kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo kwa kuongeza vitendea kazi vya kisasa ikiwa ni kuunga jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye Februari 04 Mwaka huu alipokea tuzo ya “The Gates Goalkeepers Award”

Hiyo ni kama kielelezo cha matokeo makubwa ambayo yamepatikana kwenye uongozi wake kufuatia ripoti ya utafiti wa demografia na afya ya mwaka 2022 inayoonesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80.

Naye Mratibu wa Kambi hiyo Irene Alma kutoka katika Shirika la Ujerumani la Afrika Blindenhilfe amesema wameamua kufanya kambi hiyo kutokana na kuwepo kwa wahitaji wengi wa huduma ya macho na upasuaji wa magonjwa ya mkojo ambao mara kadhaa wameshindwa Kumudu gharama za matibabu hayo.

Kwa Upande wake Daktari Bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya Mkojo Said Mauji amesema timu ya wataalamu hao imebaini uwepo wa wagonjwa wengi wa matatizo ya njia ya mkojo ikiwemo tezi dume hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Kambi ya matibabu iliyofanyika Novemba 2024.

Aidha baadhi ya wakazi wa Jimbo hilo wamemshukuru Rais Samia na Mbunge wa Jimbo hilo Geophrey Pinda ambapo wameeleza kuwa huduma hiyo imekuwa afueni kubwa kwao, hasa kwa matibabu ya kibingwa ambayo awali walishindwa kuyapata kutokana na gharama kubwa.

Ikumbukwe kuwa hii ni Kambi ya Pili ya Matibabu inafanyika Jimboni hapo ambapo kambi ya awali ilifanyika Novemba 2024 huku zaidi ya wananchi 140 wakifanyiwa upasuaji wa huduma ya macho na kambi hii ya pili itajumuisha upasuaji wa magonjwa ya njia ya Mkojo.

Rais Samia apokea tuzo maalum katika Mkutano wa ALAT
UVCCM Kagera waanzisha Samia New Voters Campaign