Katubu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi, Ally Hapi amevitaka vyama vilivyoshiriki harakati za ukombozi wa Nchi za kusini mwa Afrika vijitenge na rushwa kwa nguvu zao zote ili vyama hivyo viendelee kukubalika na kuungwa mkono na wananchi na kuendelea kubaki madarakani.
Ameyasema hayo juzi Mjini Kibaha alipokuwa akifunga mafunzo ya Viongozi wa vyama sita vilivyoshiriki harakati za ukombozi wa Nchi za kusini mwa Afrika yaliyofanyika katika shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere huko Kibaha Kwa Mfipa mkoani Pwani.
Alisema ili chama kiendelee kuungwa mkono na wananchi ni lazima kijitenge na rushwa na watu watakipenda kulingana na kazi zake na jinsi chama kinavyotenda haki kwa wananchi wake hilo linatakiwa kuzingatia na vyama vyote vya ukombozi kusini mwa Afrika.
“Adui mkubwa kwa vyama vya siasa ni rushwa viongozi endelezeni mapambano dhidi ya rushwa kwenye vyama vyenu kwani vyama hivyo ni vyama vya wananchi ambao ni wa hali ya chini kiuchumi wakiwemo wakulima wafugaji na wananchi wa kawaida hivyo zingatieni kupambana na adui rushwa kwa nguvu zao zote” alisema.
“Chama cha Mapinduzi Tumekuja na mkakati wa kudhibiti rushwa katika chaguzi za ndani ya chama ili kupata viongozi bora wenye sifa na wanaokubalika kwa jamii ambapo mgombea atajadiliwa na wajumbe mpaka zaidi ya 20000 tofauti na ilivyokuwa mwanzo alijadiliwa na wajumbe wachache”.
“Tukiendekeza rushwa kwenye vyama vyetu tutaweka pengo kati ya viongozi na wanachama wetu hadi kwa wananchi wetu, mfano hai ndani ya CCM endapo kutaonekana kuna viashiria vya rushwa chama chetu huchukua hatua mara moja kama jinsi tulivyofanya mabadiliko tulipokutana kwenye mkutano mkuu Dodoma na hivi sasa tumekuja na mkakati wa kudhibiti rushwa huwezi kuhonga watu 20,000 ambao watajadili jina la mgombea tofauti na ilivyokua zamani jina la mgombea lilijadiliwa na watu 700 tu.
“Vyama hivi vinatakiwa kuendelea kupinga rushwa tusiruhusu watu wakafika mahala na kusema chama hiki sio msemaji wetu ni lazima tujitenge na rushwa na kuwa karibu na watu wetu ambao wanatufanya kuendelea kuongoza,” alisema.
“Chama ambacho kitajipambanua kwa miongozo ya haki wananchi watakipenda, vijana ni kundi kubwa sana hivyo vyama vyetu viwajengee uwezo vijana na kuwajenga kiuzalendo wajue historia za vyama vyao na lazima kuwe na mfumo wa kubadilishana vijiti ndani ya chama tena bila mifarakano ili maono waliyokuwanayo viongozi wetu waasisi yaendelee” alisema.
Aidha aliongeza kuwa vyama hivyo vikahimarishe umoja na mshikamano baina yao katika nchi zao pamoja na kuwa karibu na watu ambao wataongeza idadi ya wanachama.
Alisema CCM itaendelea kushirikiana na vyama hivyo huku ikizingatia kuwa karibu na watu kwa kuwasikiliza na kutatua Changamoto zao jambo ambalo limefanya chama hicho kuendelea kuwa madarakani kwa kuendelee kuwa na wanachma ni lazima kuhimarisha umoja na mshikamano baina yao.
Hapi amesema kuwa agenda ya umoja ni muhimu ndani ya vyama, mrafakano mgawanyiko na makundi ndivyo huua vyama hivyo amewataka wahitimu hao kuzingatia hilo.
“Tuendelee kuangalia na kuongoza kwa kuzingatia misingi ya haki tusiweke mpasuko baina ya watu na chama”.
Kadhalika alisema vyama hivyo pia vinatakiwa kusimamia mapambano dhidi ya rushwa huku ndani na nje ya vyama vyao ili kuendelea kusimamia misingi ya haki jambo ambalo linatakiwa kusisitizwa kwa vitendo jambo litakaloongeza kuaminiwa kwenye jamii zao.
Pia Hapi alisema vijana wanatakiwa kuandaliwa kwa kupewa mafunzo ya itikadi, uzalendo na si tu kwa uongozi lengo ni kuwa na vijana ambao watakuwa viongozi wajao watakaokuwa wazalendo.
Alisema kuwa pia vijana wanajengewa uwezo ili waje kuwa viongozi bora wa baadaye ambapo viongozi ambao wameongoza wanastaafu hivyo lazima vijana waandaliwe ili wawe warithi kwani bila ya kuandaa vijana vyama hivi vitapitia changamoto.
“Mafunzo mliyojifunza yanawafanya mje kuwa viongozi bora na hii ndiyo sifa ya CCM kuandaa viongozi wake tunahakikisha wamepikwa wakaiva ili waje kuwatumikia wananchi na tunazingatia wale wenye sifa na kukubalika na wananchi,”alisema Hapi.
Mkuu wa shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Prof. Marcelina Chijoriga alisema vijana wengi walipiga katika shule hiyo na kupata mafunzo wamepata vyeo jambo ambalo ni moja ya matokeo chanya kwao.
Alisema tangu shule hiyo ianzishe zaidi ya viongozi 11,000 wamepata mafunzo huku matumaini ya shule hiyo ikiwa ni kuona wanufaika wanakuwa viongozi washirikishaji.
Vyama vilivyoshiriki mafunzo hayo ni vilivyoshiriki katika harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika ambavyo ni ANC cha Afrika kusini, FRELIMO cha Msumbiji, NPLA cha Angola, SWAPO cha Namibia, ZANU PF cha Zimbabwe na CCM kwa kushirikiana na chama Cha kikomunisti Cha nchini China CPC.