Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja ameongoza Kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kwa ajili ya kujadili aina mpya ya Gugumaji (Salvinia Spp) kilichofanyika jijini Mwanza. Kikao hicho kimewashirikisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. James Kilabuko, Makatibu Tawala wa Mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara na Taasisi.
Mambo yaliyoazimiwa katika kikao hicho pamoja na mambo mengine ni kuanza mara moja kazi ya kuyaondoa aina hiyo mpya ya magugu maji yaliyozaliana katika Ziwa Victoria. Akifunga kikao hicho, Mhandisi Luhemeja amesema hatua ya kuyaondoa magugu itatekelezwa na taasisi za Serikali, vikosi vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi.
Kikao hicho ni muendelezo wa ziara iliyofanywa na Makatibu Wakuu katika eneo la Kigongo- Busisi wilayani Misungwi mkoani Mwanza tarehe 10 Machi, 2025 ambalo limezingirwa na gugu hilo. Kukithiri kwa gugu hilo kumeleta athari mbalimbali kwa jamii ikiwemo kuharibika kwa vivuko na hivyo kutatiza usafiri wa vivuko, na athari kwa samaki.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema Ziwa Victoria linategemewa kwa kiasi kikubwa na jamii ya wananchi wanaozunguka ziwa hilo hususan wavuvi hivyo kuwepo kwa gugu maji kunaleta athari katika maisha ya jamii hiyo. Kwa mujibu wa Prof. Shemdoe asilimia 63 ya wavuvi wanategemea ziwa hilo na kufuatiwa na maziwa mengine pamoja na bahari hapa nchini hivyo zinahitajika juhudi kubwa kukabili magugu maji.

Afya Tip: Umuhimu wa Pilipili hoho Mwilini
Wakuu wa Usalama Barabarani watakiwa kusimamia Sheria