Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za Makazi za Watumishi wa Umma ikiwemo ujenzi wa Awamu ya Pili wa nyumba za watumishi 3,500 eneo la Nzuguni ‘B’ jijiini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Vumma amesema mradi huo ambao kwa sasa upo katika Awamu ya Pili ya utekelezaji wake, umeanza kwa ujenzi wa nyumba 60 za chini na maghorofa matatu ambayo kila moja litachukua familia 30.
“Mradi huu ni mkubwa, kimsingi awamu ya kwanza walijenga nyumba 150 ambazo zimekamilika na zina wapangaji zote, nyumba tumezikagua ni nzuri na ni bora sana, sasa hivi wapo katika awamu ya pili ya ujenzi wanajenga nyumba za chini na maghorofa, mradi huu kikamilika kwa awamu zote utakuwa na jumla ya nyumba 3,500”, amesema Mheshimiwa Vumma.
Aidha, Vumma Ameipongeza TBA kwa ubunifu mzuri wa mradi mkubwa na wa kimkakati ukizingatia Dodoma ni jiji linalokuwa na uhitaji wa nyumba ni mkubwa na kuusisitiza Wakala huo kuzisimamia nyumba hizo na kuzitunza ili zilete tija.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi na Umeme wa Wizara ya Ujenzi, Qs. Mwanahamisi Kitogo ameahidi kuufuatilia Wakala huo kuzisimamia nyumba hizo ili zidumu kwa muda mrefu na kuboresha utoaji huduma bora kwa wateja wake.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo pia utahusisha ubia kati ya Wakala huo na Sekta Binafsi lengo ni kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa haraka na ufanisi.
Mradi wa ujenzi wa nyumba za Makazi 3,500 eneo la Nzuguni ‘B’ jijini Dodoma unatekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ya nyumba 150 tayari imekamilika na sasa ujenzi kwa awamu ya pili unaendelea.