Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha sekta ya mifugo inakuwa endelevu na yenye tija.

Amesema kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mara zote ameweka msisitizo katika kuiendeleza sekta hiyo kwa kuwa mifugo ni uchumi, ajira na ni biashara.

Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipozungumza na wananchi katika mikutano aliyoifanya jana Jumatano (Machi 12, 2025) Wilayani Igunga, mkoani Tabora ambapo yupo kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili.

“Tunawahamasisha wafugaji, fugeni mifugo ni uchumi, mifugo ni maisha na mifugo ni pesa na wakulima limeni tupate mazao mengi ya chakula na biashara na ni lazima wafugaji na wakulima tuelewane.”

Katika hatua nyingine Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini kuweka mikakati ya kuhakikisha wanakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuzisimamia fursa zilipo kwenye maeneo yao ili kuwanufaisha wananchi. “Mkifanya hivyo mtakuwa mmewasaidia wananchi kujiendeleza kiuchumi.”

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye shule ya Sekondari ya Seif Gulamali, Majaliwa ameitaka jamii kuweka nguvu za pamoja katika kumlinda mtoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.

Majaliwa pia amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikakati iliyopo katika sekta ya elimu ili sekta hiyo iweze kuwanufaisha watanzania kwa kukuza ubora wa elimu nchini.

Kusaga ampa mwaliko maalum Rais Samia kwenye Tuzo za Malkia wa nguvu 
Maisha: Mzungu wa Facebook alivyonitapeli Dola 350