Boniface Gideon – Tanga.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Dkt. Batilda Buriani,amewaomba wadau wa Maendeleo mkoani Tanga, kujitokeza kuongeza nguvu ya uwekezaji kwenye kituo cha Sayansi Kisosora cha Stem Park Tanga chini ya Project Inspire.

Dkt.Batilda ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka mitano ya kituo hicho, baada ya kuanza kuleta matokeo makubwa kwa Wanafunzi na Vijana Wabunifu.

“Tumeona sote matokeo makubwa kwa Wanafunzi na Vijana Wabunifu,matunda tumeanza kuyaona, watoto wamefikia hatua wanabuni na kutengeneza kitu ambacho kinaweza kuisaidia jamii ,mfano tumeona Wanafunzi wameweza kubuni mfumo wa kuchuja maji machafu kuwa majisafi bila gharama kubwa, pia tumeona Wanafunzi wameweza kubuni kofia maalumu ya kumuongoza mtu mwenye ulemavu wa Macho,hii ni hatua kubwa sana katika kwa watoto wetu,” aliongeza Dkt. Batilda

Alisema wadau wa maendeleo wanatakiwa kujitokeza kuongeza nguvu hususani kwenye rasilimali fedha kama walivyofanya Halmashauri ya Jiji la Tanga ambapo imechukua asilimia 20 ya gharama za uendeshaji wa kituo hicho,

“Wadau mjitokeze kusaidia hususani kwenye rasilimali fedha,hawa ndugu zetu Project Inspire hatutokuwa nao siku zote,muda wao ukiisha wataondoka na kutuachia kituo hiki,hivyo kila mmoja wetu anaweza kuwa sehemu ya Mchango wa kituo hiki,” alisema Dkt. Batilida

Kwaupande wake Mkurugenzi wa kituo hicho, Dkt. Lwidiko Mhamilawa, alisema zaidi ya Wanafunzi 30,000 na Walimu zaidi ya 200 wamenufaika na kituo hicho.

“Ndugu wadau, wakati tunaanza kutoa huduma za Kisayansi hapa kituoni tulikuwa tunahudumia Wanafunzi 50 kwa siku ,lakini kwasasa tunauwezo tunahudumia Wanafunzi zaidi ya 200 kwa siku, ambapo hadi hivi sasa Wanafunzi zaidi ya Wanafunzi 30,000 wameshanufaika pamoja na Walimu zaidi ya 200 wamenufaika,” alisisitiza Dkt. Lwidiko

Akizungumza kwa niaba ya halmashauri ya Jiji la Tanga Naibu Meya wa Baraza la madiwani Rehema Mhina amepongeza uwepo wa kituo hicho ambao umeanza kuzaa matunda huku akiwaahidi kuendelea ushirikiano baina yao na kituo.

“Niwapongeze sana watekel zaji wa mradi huu ambao umeanza kuleta matokeo ya kuonekana tumejitahidi sana kuhamasisha watoto kupenda masomo ya sayansi katika Jiji letu la Tanga,” alisisitiza Rehema.

Buruhan awaita Vijana kushiriki uchaguzi Mkuu 2025
Nzega: Wananchi watakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi