Johansen Buberwa – Kagera.

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya imetangaza kuwa kwasasa hakuna ugonjwa wa Marburg na kuwataka Wananchi kuendelea kuwa huru katika uzalishaji wa uchumi na Maendeleo.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama ametoa kauli hiyo leo Machi 13, 2025 wakati akihitimisha shughuli zote zilizohusu mlipuko wa ugonjwa huo ulioikumba Kata ya Ruziba, Wilaya ya Biharamulo Mkoa wa Kagera Januari 16 mwaka mwaka 2025 na kusababisha idadi ya vifo vya watu wawili.

“Nachukua nafasi hii kuutangazia umma kwamba nchi ya Tanzania ni salama hakuna tena ugonjwa wa Marburg kwa sasa wananchi wawe huru kufanya shughuli zao bila wasiwasi nawasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono kwa kutumia maji safi na sabuni na vitakasa mikono ili kuendelea kuwa na afya njema na kujiepusha na magonjwa ya mlipuko,” amesema Waziri Mhagama.

Hata hivyo Waziri Mhagama amesema kuwa hii ni mara ya pili mkoa huo kupata madhara ya ugonjwa huu ambapo kwa mara ya kwanza mgonjwa wa Marburg alipatikana katika Kata ya Maruku kwenye vijiji vya Burinda na Butayaibega Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera mwaka 2023 hivyo uwepo wa ugonjwa huo mara mbili mfululizo kumeifanya serikali kuchukua hatua kadhaa ili kuhakikisha inakabiliana na ugonjwa wa mlipuko.

Mganga mkuu wa serikali Dkt Grece Magembe amesema mnamo januari 21 Rais Dkt Samia Hassan akitangaza kuwepo kwa ugonjwa huo na kufikia 28 januari 2025 idadi ya watu wawili walithibitika kuwa na maambukizi na wote walifariki dunia ambapo kuna baadhi ya watu tangamana nao 281 na Kati ya hao wahudumu wa afya walikuwa 64 na waliwekwa karantini na wameweza kutoka salama February 10 mwaka huu.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mwandisi Ezra Chiwelesa ameishukuru serikali kwa juhudi kubwa za kukabiliana na ugonjwa huo na kuiomba Serikali iwaangalie kwa jicho la pili wahudumu waliojitolea kuihudumia jamii kupata ajira kwa muda wa miaka mitano kutokana na kazi kubwa iliyofanyiwa nao.

Buruhan awaita Vijana kushiriki uchaguzi Mkuu 2025