Mahakama ya Wilaya Sengerema, mkoani Mwanza, imemuhukumu Lucas Maselele (56), mkazi wa kijiji cha Lugata, kwenda jela miaka 30 baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mjukuu (13).

Hukumu hiyo, ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Evod Kisoka katika kesi ya jinai namba 16492/2024.

Awali, Mwendesha Mashtaka, wakili wa Serikali Nyamhanga Tissoro, aliieleza mahakama kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe Juni 4, 2024, katika kijiji cha Lugata. Alidai kuwa Lucas Maselele alimbaka mjukuu wake wakati mke wake alipokuwa msibani. Alifumaniwa na mke wake akifanya kitendo hicho, kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(e) pamoja na 131(1) vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 14, 2024 baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi na kusomewa shitaka hilo, ambapo alikana.

Upande wa Jamhuri ulileta ushahidi, na shauri lilianza kusikilizwa katika mahakama hiyo na Lucas alijitetea na kuomba mahakama imuachie huru, akidai kuwa ni njama zilizotengenezwa na mke wake.

Hata hivyo, mahakama baada ya kupitia vifungu vya sheria sambamba na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri, ikiwemo ripoti ya daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, imejiridhisha kuwa upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha shtaka hilo bila ya kuacha shaka yoyote.

Katika uamuzi wake, mahakama ilithibitisha kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo la kumbaka mjukuu wake na hivyo kumuhukumu kwenda jela kwa miaka 30.

Afya Tip: Dalili za ugonjwa wa baridi yabisi na tiba yake
Mamlaka Serikali za Mitaa zapewa maagizo