Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendesha mafunzo kwa watumishi wa umma, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa jinsi ya kutumia moduli ndogo za Mfumo wa NeST zilizoongezwa hivi karibuni, za upekuzi wa mikataba na majadiliano. Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia Machi 10-14, 2025, jijini Arusha.

Meneja wa Mafunzo na Kujenga Uwezo wa PPRA, Bw. Gilbert Kamnde amesema kwakua Mfumo wa NeST umeendelea kuboreshwa na hivi sasa upekuzi wa mikataba (contract vetting) na majadiliano (negotiation) vinafanyika ndani ya Mfumo huo, Mamlaka hiyo imeanza kuwajengea uwezo watendaji ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.

Washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza Mamlaka kwa kuendelea kutoa mafunzo, wakieleza kuwa Mfumo wa NeST unavyoendelea kuboresha unawaongezea ufanisi na kuwapunguzia hoja za kikaguzi, ili kuwahudumia wananchi.

Kaimu Mkurugenzi, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira – Njombe, Mhandisi Robert Lupodya aliyehudhuria mafunzo hayo, amesema elimu aliyoipata itamsaidia katika kusimamia ipasavyo majadiliano na kufuatilia upekuzi wa mikataba kwenye Mfumo, hatua inayomuongezea ufanisi katika kusimamia shughuli za taasisi yake.

“Mimi binafsi ninakubali kwamba Mfumo huu utatusaidia sana sisi watanzania, hususan sisi taasisi nunuzi. Hii ina maana kwamba itatusaidia kupunguza gharama na kuongeza ufanisi wa usimamizi wa matumizi ya fedha na uzingatiaji wa sheria. Huu Mfumo unatengeneza ushindani wa wazi, na hivyo unatusaidia kupata thamani halisi ya fedha,” Mhandisi Robert.

Naye Mkurugenzi wa Ununuzi wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Bi. Metrida Kaijage, amesema kuwa Mfumo wa NeST umeongeza imani kwa wazabuni hususan katika uandaaji wa nyaraka.

“Kwa sababu sasa hivi nyaraka zote zinapatikana kwenye Mfumo, wazabuni wana imani. Lakini pia tulikuwa tunatumia muda mrefu kuandaa nyaraka na kupata ridhaa. Lakini sasa hivi imetusaidia kupunguza muda na kuondoa hoja za ukaguzi,” amesema Bi. Kaijage.

Bi. Kaijage amempongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza nguvu zaidi kwenye matumizi ya mifumo, hatua iliyosababisha hata taasisi za kimataifa kuridhia miradi yao kutekelezwa kupitia Mfumo wa NeST.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na watumishi wa ngazi zote, wakiwemo wakuu wa taasisi, maafisa ununuzi, wanasheria wa taasisi nunuzi na kada nyingine.

Ukusanyaji wa Mapato: Sangaiwe mfano wa kuigwa - DC Kaganda