Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imepongeza viwango vya ubora wa ujenzi wa mwalo wa Chato Beach uliopo Wilaya ya Chato mkoani Geita ambao umefikia asilimia 91 hadi kukamilika kwake.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deodatus Mwanyika mara baada ya kuiongoza kutembelea na kukagua ujenzi wa mwalo huo ambapo ametoa rai kwa Taasisi nyingine za Serikali kutafuta wakandarasi wenye sifa za aina hiyo.

“Mara nyingi huwa tuna mjadala mrefu sana tunapotembelea miradi ya aina hii lakini leo tumekaukiwa maneno kwa sababu tumekutana na mradi tuliothibitisha kweli umekamilika kwa asilimia 91,” aliongeza Mwanyika.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na watendaji wake kuhakikisha wanampa miradi mingine ya wizara mkandarasi huyo kutokana na kazi aliyoifanya kwenye ujenzi wa mwalo huo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa mara baada ya kukamilika kwa mwalo huo, wataalam kutoka chuo cha mafunzo ya Uvuvi nchini (FETA) watafika kutoa elimu ya namna ya kufanya shughuli zao kitaalam mwenye mwalo huo.