Malipo ya mkupuo wa awali wa Mafao yameongezeka asilimia 69, kutoka TShs bilioni 537.08 huku kiwango cha kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kimeboreshwa katika kipindi husika.

Akizungumza na Waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa hifadhi ya Jamii ( NSSF), Masha Mshomba leo Machi 17,2025 Jijini Dodoma ambapo amesema malipo ya mafao kwa mwaka yaliongezeka kwa asilimia 69 kutoka TZS bilioni 537.08 na katika mwaka ulioishia Februari 2021 hadi kufikia TZS bilioni 909.16 katika mwaka ulioishia Februari 2025.

“Mfuko ulilipa mafao ya TZS bilioni 3,108.89, na Vilevile, kutokana na mabadiliko ya kanuni ya ulipaji mafao ya kustaafu (kikokotoo) yaliyofanyika na kuanza kutekelezwa mwezi Julai 2022, wastaafu wa NSSF walianza kupokea mkupuo wa awali wa asilimia 33 ukilinganisha na asilimia 25 waliyokuwa wakilipwa kabla ya mabadiliko hayo”,

“Aidha, kutokana na utendaji uliotukuka wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwajali wastaafu, Mfuko umeendelea kuboresha tena ulipaji wa mafao kwa wanachama wote waliokuwa wanalipwa mkupuo wa awali wa asilimia 33 na kwanzia mwezi Julai 2022, waliongezewa kiwango cha mkupuo kufikia asilimia 35”. Amesema Mshomba.

Amesema uamuzi huo wa Serikali wa kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kwa wanachama wa NSSF pia umezingatia uendelevu wa Mfuko.

Hata hivyo amesema Mfuko upo kwenye hatua za mwisho za kuboresha kiwango cha kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu kutoka TZS 100,000 hadi
TZS 150,000.

“Viwango vingine vya pensheni vinatarajiwa pia kuongezeka kwa asilimia 2 na asilimia 20, Utekelezaji wake utaanza mara moja baada ya taratibu za uidhinishwaji kukamilika na utahusisha kipindi cha kuanzia tarehe 1 Januari 2025”, amesema

Hata hivyo amesema maboresho ya huduma na matumizi ya TEHAMA yamepewa kipaumbele.

“Mfuko umefanya maboresho mbalimbali katika utendaji ili kuwawezesha
wanachama kupata huduma mbalimbali kwa urahisi na kupunguza usumbufu, Moja ya hatua hizo ni kuanzishwa kwa mikoa mipya ya huduma Ubungo na Kigamboni jijini Dar es Salaam pamoja na kupandisha hadhi vituo vitatu vya Mkuranga,Hai na Mbezi Beach kuwa na hadhi ya ofisi za wilaya”, amesema

“Kwa kuzingatia kwamba matumizi ya TEHAMA ni moja ya maeneo yanayotiliwa
mkazo na Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko pia umebainisha eneo hili kama eneo la kipaumbele ambapo baadhi ya maboresho ya mifumo yamewezesha waajiri na wanachama wa Mfuko kujihudumia na kupata huduma mbalimbali kupitia mifumo ya TEHAMA pasipo kulazimika kufika katika ofisi za Mfuko”. Amesema Mshomba.

Ameongezea kwa kusema Matumizi ya TEHAMA katika utendaji wa Mfuko yameongeza kutoka asilimia 48
iliyokuwa imefikiwa mwezi Februari 2021, hadi kufikia asilimia 87.5 Februari 2025, ikitarajiwa kufikia asilimia 100 ifikapo Juni 2025.

Serikali yaweka mazingira rafiki kwa Wanasayansi na wabunifu
Maisha: Nilivyomshinda tapeli wa viwanja kirahisi