Bohari ya Dawa Nchini (MSD), imesema inatekeleza mpango maalumu wa kuongeza upatikanaji wa huduma za uchujaji wa damu ikiwa ni sehemu ya matibabu ya figo, kwa lengo la kupunguza gharama za huduma hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Machi 19, 1015 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali hadi kufikia mwezi Februari 2025, idadi ya mashine imeongezeka na
kufikia 137 kutoka mashine 60.

Amesema ongezeko hilo limefanya idadi ya hospitali zilizopokea mashine kutoka Bohari ya Dawa kutoka Hospitali sita zilizokuwepo mwaka wa fedha 2021/22 kufikia 15 kwa mwaka 2024/25.

“Uwekezaji huu uliofanyika umegharimu
kiasi cha shilingi bilioni 7.7 katika Hospitali hizi, Hospitali 11 zimeanza kutoa huduma na hospitali 4 zipo katika hatua ya matengenezo,” amesema Tukai.

Amezitaja baadhi ya Hospitali zinazotoa huduma hizo kuwa ni pamoja na zile za Rufaa za Mikoa ya Amana, Mwananyamala ,Temeke, Morogoro, Katavi, Tumbi, Chato, Sekoe Toure na UDOM Hospitali.

Aidha, Tukai amesema mkakati wa usambazaji wa mashine hizo pia unalenga kupunguza gharama ambayo ni kati ya shilingi 200,000 na shilingi 230,000 na matarajio ni kuweza kupunguza na kuwa chini ya shilingi 100,000 kwa awamu moja.

“Mkakati huu unatekelezwa chini ya uratibu imara wa Wizara ya Afya kwa kushirkiana na hospitali zinazotoa huduma za hemodialysis ambapo kifurushi cha msingi cha vifaa vinavyotumika katika hemodialysis kwa ajili ya vipindi 100 (hemodialysis consumables basic kit content for 100 sessions) kimeanzishwa,” amesema.

Kuhusu usambazaji wa bidhaa za afya ya kinywa na meno, Tukai amesema umeendelea kuimarika katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita ambapo Bohari ya Dawa imeendelea kuhakikisha bidhaa
za afya ya kinywa na meno zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Bohari ya dawa imesambaza bidhaa
za afya za kinywa na meno zenye thamani ya shilingi bilioni 9.98 kutoka kusambaza
bidhaa za afya za kinywa na meno zenye thamani ya shilingi milioni 254.7 kwa mwaka 2021/2022,” alifafanua zaidi.

Ameogeza kuwa, “Katika kipindi cha miaka minne mfululizo bidhaa za afya za kinywa na meno zenye thamani ya shilingi bilioni 21.5 zimesambazwa, ambapo shilingi bilioni 17.87 ni thamani ya viti vya kutolea huduma za kinywa na meno na pamoja na mashine za mionzi ya kinywa na meno ambayo ni sawa na asilimia 83.”

“Katika gharama hii, viti vya huduma za kinywa na meno vimegharimu shiling bilioni 13.8 na kuwezesha kusambazwa kwa viti 647 na mashine za kisasa za mionzi za kinywa na meno zikiwa ni 331 zenye thamani ya shilingi bilioni 4.07. Bidhaa hizi zimesambazwa katika hospitali,” aliainisha Tukai.

Dkt. Biteko ataka upotevu wa Maji udhibitiwe
Manyara: THBUB yawataka Wananchi kufichua uvunjifu haki za Binadamu