Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema jamii inahitaji kufundishwa, kutambua na kuenzi mila za Kitanzania, pamoja na kujiepusha na vishawishi vya kuiga tabia za kigeni ambazo hazina manufaa kwa ustawi wa Taifa.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Machi 19, 2025 katika Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Msaidizi Mstaafu wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Bukoba Askofu Method Kilaini.

Amesema, “sote tumekua tukishuhudia ongezeko la vitendo vya ukosefu wa maadili katika jamii. Vitendo hivi vinatokana na malezi hafifu lakini pia watu kuiga mila na desturi kutoka mataifa mengine ambazo haziendani na tamaduni na maadili yetu ya Kitanzania.”

Waziri Mkuu amesema hali hiyo imeathiri mwenendo wa jamii, hususan kwa vijana ambapo wanashuhudia mabadiliko katika misingi ya familia, jamii, na Taifa kwa ujumla. “Nitumie fursa hii kuliomba Kanisa kuendelea kuwa nguzo ya maadili bora, kwa kutoa mwongozo wa kiroho na kijamii.”

Amesema Kanisa lina nafasi ya pekee katika kuhakikisha Taifa linarudisha maadili ya kweli ya Kitanzania yanayofundisha kuheshimu utu, haki, na amani. “Serikali, tunatambua mchango mkubwa wa Kanisa katika hili na tutashirikiana nalo ili kuleta mabadiliko chanya kwa kizazi cha sasa na kijacho.”

Majaliwa amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa madhebu ya dini ikiwemo Kanisa Katoliki katika kuboresha ustawi wa jamii.amii yetu., hivyo amewaomba viongozi wa dini nchini waendelee kuwa nguzo ya maadili bora, kwa kutoa mwongozo wa kiroho na kijamii.

Akizungumza kuhusu Askofu Kilaini, Mheshimiwa Majaliwa amesema ni kielelezo cha ujasiri, imani thabiti, na huduma ya kujitolea kwa Kanisa na jamii ya Watanzania, ameonesha nguvu ya uvumilivu, akiwa na michango mikubwa katika maisha ya kanisa.

Amesema pamoja na changamoto nyingi alizokutana nazo, hakukata tamaa, bali aliendelea kuwa mwanga kwa wengi. “Ninatambua kuwa katika kipindi cha uongozi wake, alifanya kazi muhimu katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akiwa Katibu Mkuu kwa miaka tisa na nusu, akisaidia kuimarisha huduma za jamii na kuendeleza taasisi mbalimbali za Kanisa, ikiwemo hospitali ya Bugando na Chuo Kikuu cha Nyegezi.”

“Kama Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alijizatiti katika kuimarisha utawala wa fedha za Kanisa na kusaidia kuanzisha Radio Tumaini, hatua muhimu katika mawasiliano ya kiroho. Kwa ushirikiano wake na viongozi wa Kanisa, alisaidia pia kuanzisha Television ya Tumaini, akionesha uongozi wa kimapokeo na kisasa.”

Akimzungumzia Askofu Msaidizi Mstaafu. Method Kilaini Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa amesema Askofu huyo ni hazina kubwa ya mkoa wa Kagera kwani licha ya kutoa huduma za kiroho mara nyingi amekuwa akishiriki katika matukio mabalimbali yanayofanywa na Serikali. “Amekuwa mshauri mzuri katika masula mbalimbali hasa yanayohusu amani na maendeleo ya Taifa letu.”

Naye, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu Angelo Accaltino amesema anafurahishwa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya kanisa Katoliki na Serikali ya Tanzania na uwepo wa Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Jubilei hiyo ni ushahidi. “Natamani kuona ushirikiano huu unadumu na kuendelea kukua.”

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi Method Kilaini amesema anamshukuru Mungu kati ya mambo mengi aliyoyafanya aliguswa sana na ushirikiano alioupata kutoka kwa Sheikh wa Mkoa wa Kagera Haruna Kichwabute katika kutafuta amani na maridhiano kati ya Wakristo na Waislamu mkoani Kagera.

“Tumefanikiwa sana kuwaunganisha Wakristo na Waislamu mkoani kwetu, sisi ni ndugu sisi ni wamoja na ndio maana leo hii namuona Sheikh wetu wa Mkoa yupo hapa kanisani akishirikiana nasi katika Jubilei hii.”

Dkt. Biteko ataka upotevu wa Maji udhibitiwe