Matumizi taarifa za Takwimu: NBS yawanoa Maafisa Habari Kanda ya Ziwa
11 hours ago
Katika kuboresha usimamizi na usambazaji wa Takwimu sahihi katika jamii, Ofisi ya Takwimu Taifa (NBS) imefanya mafunzo kwa Maafisa Habari wa Halmashauri, Wilaya na mikoa ya Kanda ya Ziwa, ili kuwapa uelewa juu ya namna ya kuzitumia katika kutoa taarifa za kimaendeleo.
Akizungumza katika semina iliyowakutanisha Maafisa hao Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, Mratibu wa mafunzo hayo Said Hemedi amesema Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa ya kutafuta takwimu ambazo zinatakiwa kutumika katika kufanya maamuzi ya kisera hivyo ni haki ya kila mtumiaji kuzifahamu hususan maafisa habari ambao hutakiwa kuweka wazi ili mwananchi ajue utekelezaji wa miradi na idadi ya wakaazi husika.
“Hizi takwimu tunazipata kwa njia ya sensa ya watu na makazi kuanzia ngazi ya kaya kwa gharama kubwa sasa taasisi zote zinazotumia takwimu zinatakawa kuzitumia ipasavyo ili pale tunapotoa ripoti za maendeleo ya halmashauri zetu kwamba serikali imefanya nini tuhusishe moja kwa moja na takwimu,” alisema Mratibu Said.
Kwa upande wake Afisa Habari Mkoa wa Simiyu, John Mganga ameishukuru ofisi hiyo kwa kutoa elimu huku akiahidi kuyatumia ipasavyo mafunzo hayo katika kuhabarisha uma na kuyapandisha katika tovuti za mikoa ili ajenda za kiserikali ziifikie jamii kwa urahisi.
“Aipekee niishukuru ofisi ya takwimu kwa mafunzo haya na niahidi tu tunakwenda kuyatumia ipasavyo katika kutoa taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika halmashauri zetu na kuzipandisha katika tovuti zetu ili kusiwe na maswali tena kwa jamii,” alisema Mganga.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Wilaya ya Meatu, Isdory Mgoroka amesema kwasasa jamii imekuwa ikihoji juu ya takwimu, ili kuonesha ukubwa wa jambo lililofanyika hasa pale ambapo fedha za serikali zimetumika hivyo ni wazi kuwa takwimu zikitumika vizuri zitaisaidia jamii kupunguza maswali katika miradi yao.
“Watu huwa wanahoji juu ya takwimu na wakisikia tu kuna fedha zimetoka labda katika ujenzi wa shule wanataka kujua hiyo shule itachukua wanafunzi wangapi kwa hiyo hii itaturahisishia katika kila mradi wa maendeleo tutazitumia hizi takwimu kupunguza maswali kwa jamii kwa sababu kila kitu kitakuwa wazi,” aliongeza Mgoroka.
Mafunzo hayo, yamewakutanisha Maafisa wa Halmashauri na Wilaya za Mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Mara na Kagera.