Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kuwa mstari wa mbele katika kutangaza amani, upendo, maadili, na usawa miongoni mwa wananchi wa Tanzania bila kujali tofauti zao za kiimani, kisiasa, au kijamii.
Bashungwa ameeleza hayo jijini Dar es Salaam wakati alipomwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika Futari ya Viongozi wa Dini na Wadau wa Amani Tanzania iliyoandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania.
“Serikali inajivunia mchango mkubwa ambao Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) inautoa katika kuhakikisha kuwa tunaendelea kuwa na jamii iliyo na amani na utulivu pasipo kujali tofauti zetu za kiimani, kiitikadi, na kiutamaduni,” amesema Bashungwa.
Bashungwa amesema JMAT ni jumuiya inayoamini katika maridhiano ikiwa ni falsafa ya 4R ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo amekuwa akiisisitiza ili kuendelea kujenga jamii yenye upendo, amani, na mshikamano.
Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa waumini wa dini zote kuendelea kutenda mambo mema, hususan katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Mfungo wa Kwaresima, kwani ni kipindi cha kufanya toba lakini pia kuwakumbuka wahitaji na kutoa sadaka.
“Ninaomba kutoa rai kwa waumini wa dini zote kuwa mambo mema tunayoyatenda katika kipindi hiki yaendelee kuwa sehemu ya maisha yetu hata baada ya kipindi hiki cha mfungo kuisha. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na jamii iliyo bora na kuendelea kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani.” amesema Bashungwa
Kadhalika, Bashungwa ametoa pongezi kwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kudumisha na kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kutamalaki katika nchi ya Tanzania.
Naye, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakary Zubeiry bin Ally, aliwasihi wananchi kuendelea kulinda amani na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi. Pia aliwahimiza viongozi wa dini kuendeleza mahubiri ya amani wanapokuwa katika nyumba zao za ibada.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum, aliongoza hafla ya utoaji wa tuzo za heshima kwa viongozi mbalimbali, wakiwemo waasisi wa jumuiya hiyo, akiwemo Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete, na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.