Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda amewataka Watendaji wa Vijiji vinavyopakana na Hifadhi kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu kulima mazao yasiyowavutia Wanyama waharibifu ili kuepusha migogoro kati ya Binadamu na Wanyamapori.

Ametoa wito huo wakati wa hafla ya kukabidhi magunia 309 ya mahindi kwa Vijiji 10 vinavyopakana na hifadhi, mahindi ambayo yamenunuliwa na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU), kwa ajili ya wanachama waliokubali kushiriki kwenye uhifadhi.

Mahindi hayo yamegawiwa kwa shule mbalimbali za msingi zilizopo katika kata za Mwada, Nkaiti, na Magara, ili kusaidia chakula cha mchana kwa wanafunzi. Kaganda ameagiza wanafunzi waelimishwe kuhusu namna chakula hicho kilivyopatikana ili wapate uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.

Aidha Kaganda ameeleza kuwa uelewa huu utasaidia kujenga kizazi chenye kuthamini rasilimali za asili na kushiriki kikamilifu katika jitihada za uhifadhi.

Kaganda amesisitiza umuhimu wa kuandaliwa mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa vijiji vinavyopakana na hifadhi ili kuweka mipaka bayana kati ya shughuli za kilimo na maeneo ya uhifadhi.

Amesema kuwa mipango bora ya matumizi ya ardhi itaondoa migogoro kati ya wakulima, wafugaji, na sekta ya uhifadhi. Pia amewataka wananchi kulima mazao kama tumbaku, ufuta, na aina maalum ya alizeti ambayo hayawavutii wanyama waharibifu.

Diwani wa Nkaiti, Steven Saruni Mollel amepongeza juhudi za JUHIBU na kusema kuwa jumuiya hiyo imeleta manufaa makubwa kwa wananchi, ambao sasa wanaelewa thamani ya uhifadhi.

amesema hatua ya kugawa mahindi hayo itasaidia wazazi na walezi katika kugharamia chakula cha mchana kwa wanafunzi, hasa kutokana na kupungua kwa shughuli za kilimo kwenye vijiji hivyo kutokana na uwekezaji katika uhifadhi.

Mafunzo ya Urubani: NIT yakamilisha taratibu kupata Ithibati ya TCAA
Serikali inatambua mchango wa Jumuiya ya Maridhiano - Bashungwa