Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya amesema Serikali imekiwezesha chuo hicho kukamilisha maandalizi ya utoaji wa mafunzo ya Urubani ambapo kimekamilisha matakwa ya kupata ithibati kutoka TCAA na hivyo mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza mwezi Mei 2025.
Dkt. Mgaya ameyamesema leo Machi 20,2025 hapa Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa chuo hicho katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Ifahamike kuwa kama nchi tumekuwa tukitegemea kwa kiasi kikubwa kupelekea watanzania kupata mafunzo ya urubani nje ya nchi, hivyo Serikali na watanzania kwa ujumla tumekuwa tukitumia fedha nyingi sana za kigeni kusomesha marubani nje ya nchi.

Amesema kwa kuanzisha mafunzo hayo hapa nchini kutapunguza gharama ya mafunzo kwa takribani asilimia 50 – 60 ambazo watanzania wengi wanatumia kupata mafunzo hayo nje ya nchi na kuongeza kuwa kuanza kwa mafunzo hayo pia kutaokoa fedha za kigeni ambazo zimekuwa zikitumika kwenda kusomesha marubani nje ya nchi.
“Kuanza kwa mafunzo haya kutaongeza idadi ya marubani wazawa hivyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi kwa marubani wa kigeni waliokuwa wanakuja nchini kufanya kazi na gharama huwa ni kubwa sana,” amesema.
Vilevile amesema Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo aina ya Cesna 172 zenye injini moja ambazo tayari zipo nchini kwaajili ya kuanza mafunzo hayo.
“Ndege hizi zina thamani bil 2.9 na Serikali ipo katika taratibu za ununuzi wa ndege nyingine tatu ikiwa ndege moja ya injini mbili ambayo itawasili mwezi Oktoba 2025 ambayo ina thamani ya bil.5.9, na Ndege mbili za injini moja zitawasili mwaka 2026.

Pia amesema Serikali imetoa eneo lenye ukubwa wa Ekari 60 katika kiwanja cha KIA mahsusi kwaajili ya mafunzo hayo ambapo ujenzi wa miundombinu unaendelea.
Pamoja na hayo Dkt.Mgaya amesema Chuo hicho kinatekeleza Mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki, ujulikanao kama “East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP)”.
Amesema kupitia mradi huo, NIT itapokea Dola za Kimarekani Mil.21,250,000 sawa na shillingi za Kitanzania bil.49 kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji (Center of Excellence in Aviation and Transport Operations – CoEATO).
“Kupitia Mradi huo Serikali imekiwezesha Chuo kujenga majengo Matano katika Kampasi ya Mabibo -Dar es salaam ambao ujenzi wake kwa ujumla umefikia asilimia 97.
“Ujenzi huu utakamilika ifikapo mwezi June 2025.Gharama ya ujenzi wa majengo haya ni bil.24.9 ambapo mradi huu umefadhili ujenzi wa jengo la mafunzo ya urubani katika eneo la KIA ambalo Serikali imetoa,” amesema Dkt. Mgaya.