Ofisi ya Makamu wa Rais imezikumbusha Wizara za kisekta kuhusu wajibu walionao katika kufungamanisha taarifa za mazingira wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili kuharakisha ukuaji wa shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi wakati akifungua kikao kazi cha kukuza uelewa kwa wadau wa Wizara za kisekta kuhusu uandaaji wa mfumo jumuishi wa usimamizi wa mazingira nchini.
Mitawi amesema mazingira ni sekta mtambuka inayogusa Wizara zote za kisekta ndani ya Serikali na hivyo upo umuhimu wa kuandaa mfumo jumuishi utakaorahisisha upatikanaji wa taarifa zitakazosaidia taifa kubaini changamoto za mazingira na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.
“Sote ni mashahidi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi zilizopo kwa sasa duniani na Tanzania kwa ujumla ambazo zimegusa sekta zote muhimu za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, fedha n.k…hivyo hatuna budi kuimarisha ushirikiano” amesema Mitawi.
Aidha Mitawi amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imekusudua kuanzisha mfumo huo wa ukusanyaji wa taarifa za mazingira ikiwa ni hatua muhimu ya kurahisisha na kuimarisha sekta ya hifadhi ya mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa Wizara za kisekta zimekuwa zikitekeleza majukumu mbalimbali kuhusu uhifadhi wa mazingira lakini zimeshindwa kuwa na mfumo wa utambuzi na kusababisha ukosefu wa taarifa na muhimu pindi zinapohitajika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya usimamizi wa mazingira Sura 191 kifungu 175 Ofisi ya Makamu wa Rais, imepewa jukumu la kusimamia mchakato wa ukusanyaji wa taarifa za mazingira nchini ambazo zimekuwa zikitumika katika majukwaa na mikutano mbalimbali ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Mitawi amesema uandaaji wa mfumo jumuishi utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza hapo awali kuhusiana na upatikanaji wa taarifa za mazingira, na hivyo kuzitaka Wizara za kisekta kutoa ushauri, maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha mfumo huo.
Kwa upande Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Paul Deogratius amesema mfumo huo umekuja kwa wakati mwafaka kwani utawezesha taarifa mbalimbali za mbalimbali katika Wizara za kisekta kuweza kusomana na hivyo kusaidia katika mipango ya maendeleo.
“Mwaka 2022 tulipoandaa Mpango Kabambe wa Mazingira tulipata taarifa mbalimbali za Wizara za kisekta katika eneo machache na hivyo kuwepo kwa mfumo huu kutasaidia upatikanaji wa taarifa za mazingira nchini” amesema Dkt. Paul.
Amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya kazi nzuri kuhusu masuala ya uhifadhi wa mazingira lakini zimeshindwa kuripotiwa na kuonekana kutokana na ukosefu wa mfumo sahihi wa utunzaji na uhifadhi wa taarifa hizo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Ofisi ya Makamu wa Rais, Joyce Mnunguli amesema Ofisi hiyo imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukamilisha mfumo huo ambao utasaidia kujibu changamoto mbalimbali za ukosefu wa taarifa za mazingira nchini.
“Ofisi inashirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na wadau wengine katika uandaaji wa mfumo na mpaka sasa tumeandaa andiko na tunaendelea na uandaaji na utayarishaji wa nyaraka mbalimbali zitakazotumika katika mfumo huu” amesema Bi. Mnunguli.