Muziki wa singeli umeendelea kukua kwa kasi kubwa Nchini na kupendwa zaidi nje ya Nje ya mipaka ya Tanzania.
Kauli hiyo, imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu na msimamizi wa Hakimiliki, Doreen Sinare ambaye amedai hata Dkt. Samia Suluhu Hassan alieleza namna alivyoshuhudia wazungu wakifurahia Muziki huo.
Amesema, “katika kipindi hiki, COSOTA imetoa elimu kwa Wasanii, watayarishaji, wafanyabiasha na wadau wa Singeli kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Uswazi Got Talent na Kandoro Baba Entertainment chini ya Meneja Kandoro kuwaeleza umuhimu wa usajili wa kazi zao na faida za kusajili ambapo takribani wasanii 20 wa Muziki wa Singeli wamesajili kazi zao COSOTA.”
“Pia wamenufaika na mgao wa mirabaha kwa mwaka 2022 na mwaka 2023 na nimategemeo yetu kuwa watanufaika Zaidi kutokana na kupendwa na kushiriki katika biashara ya muziki wa singeli ndani na nje ya nchi,” aliongeza Sinare.
Hata hivyo, amesema Serikali kupitia Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ilihaidi kuimarisha usimamizi wa hakimiliki na kuhakikisha Wasanii wananufaika zaidi na kazi zao pamoja na kupata mirabaha na ametekeleza.
“Kati ya mambo yaliyofanyika ni pamoja na marekebisho katika Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999 yaliyofanyika mwaka 2022 na 2023 kupitia Sheria za Fedha za mwaka 2022 na 2023,” amesema.
Sinare amesema mabadiliko hayo makubwa yalianzisha chanzo kipya cha mapato cha tozo ya hakimiliki (copyright levy), ambapo vifaa vinavyotumika kusambaza, kuzalisha na kuhifadhi kazi za sanaa na fasihi hutozwa asilimia moja nukta tano (1.5%) kila vinapoingia, kuzalishwa au kuundwa hapa nchini.
Amesema fedha hizo hukusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwamba lengo kuu la kuanzishwa kwa tozo hiyo ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi wadau wa sanaa na uandishi nchini wakiwemo wasanii, waandishi na wabunifu.
Kwa muda mrefu kazi zao zimekuwa zikitumika katika mazingira mbali mbali ya kijamii kama vile kuhifadhi, kubebea na kusambaza kazi sanaa na uandishi na kuwanufaisha wadau wengine pamoja na watu binafsi bila ya wenye kazi kupata haki zao.
“Marekebisho hayo ya Sheria yaliweza kuweka asilimia 1.5 kwa baadhi ya orodha ya vifaa yaani Radio/TV set enabling recording, analogue audio recorders, analogue video recorders, CD/DVD copier, digital jukebox, MP 3 player, CD, DVD, Vinyl, Mini Disc na SD Memory ili kuweza kulipishwa tozo hiyo ambapo ni vifaa 13 kati ya vifaa 25 vilivyoombwa,” amesema Sinare.