Wakala wa usajili wa Leseni na Biashara Nchini (BRELA), umetoa sadaka ya Iftar na kufuturu pamoja na Watoto yatima na wenye uhitaji, katika kituo cha Tuwalee Yatima Tanzania (TUYATA), kilichopo eneo la Magomeni Kagera jijini Dra es Salaam.
Iftar hiyo maalum, ambayo imetolewa usiku wa Machi 21, 2025 ni utaratibu wa kawaida katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kushirikiana na jamii kuwakunbuka wenye uhitaji na makundi hayo maalum.
Akiongea na Vyombo vya Habari wakati wa tukio hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa amesema lengo kuu la kutoa sadaka ya iftari ni kurudisha fadhila kwa jamii ikiwa ni sehemu ya walichokipata toka kwa Wananchi na itaendelea kutenga bajeti kila mwaka.
Amesema, BRELA itagharamia safari ya watoto hao kwenda Dodoma kwa SGR kujifunza na kuona miradi ya Serikali huku akiwapongeza Waislam wote waliofunga kwani wanakamilisha nguzo ya nne ya uislam na kufanya mambo mema yanayompendeza Mungu.
Hafla hiyo, imehudhuriwa na wadau mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mwenyekiti wa Bodi ya BRELA Profesa Neema Mori, Muwakilishi wa Mufti, katibu wa Bakwata wa Wilaya Alhaji Nuhu Jabir Mruma.
Wengine ni Shekh wa Wilaya Mohamed Ahmed Mahenga, Mtendaji wa kata ya Ndugumbi Pamela Kalungano, Menejimenti ya Brela, watumishi wa Brela, walezi wa kituo pamoja na Wananchi.
Aidha Nyaisa amewataka Wananchi kuendeleza amani, upendo na mshikamano uliopo Nchini na isiishie mwezi wa Ramadhani pekee huku akisema BRELA itaendelea kusimamia misingi ya haki, wema na ufanyaji biashara wenye kuzingatia usawa na ushindani.
Mablinna Iftar hiyo pia BRELA ilikabidhi mahitaji kituoni hapo ambayo ni kilo 500 za mchele, kilo 100 za Sukari, Magodoro 10, Unga kilo 50, Maharage kilo 50, Mafuta lita 20, Nyama kilo 20, Taulo za kike boksi 2, Sabuni na Chumvi, vyote vikowa na vyenye thamani ya Tshs Milioni 4,000,000.
Naye Bi Faudhia Jabir, ambaye ni muanzilishi wa kituo hicho cha TUYATA chenye jumla ya Watoto 225 amesema wamefaulu katuka eneo la elimu, lakini bado kunachangamoto ya makazi ya watoto wengi yatima.
Aidha, ameomba kusaidiwa ili kuawajengea nyumba za kuishi pamoja na wajane, ili nao waweze kujitegemea na wajiingizie kipato na kuendesha maisha yao wenyewe kwani wanazo Ekari zaidi ya 20 kwa ajili ya kufanikisha azma hiyo.