Tangu kuanza kwa uendeshaji wa Reli ya SGR kumekuwepo na matukio mbalimbali ya uhujumu wa miundombinu ya reli yaliyopelekea kukosekana kwa huduma ya usafiri kwa masaa kadhaa na kusababisha adha kwa watumiaji wa hudumu za reli ya SGR.
Akizungumza na Waandishi wa habari Leo Machi 22,2025 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa ambapo amesema wizi wa nyaya za shaba (copper wire) zenye uzito unaofikia Kilogramu 21,819.3 na vifaa vingine uliotokea maeneo mbalimbali na kwa nyakati tofauti kati ya Dar es salaam na Dodoma.
“Urushiaji wa mawe treni wakati wa treni zinafanya safari zake, jumla ya matukio makubwa mawili yalitokea na kupelekea kuvunjwa kwa vioo vya mabehewa, Kukata uzio wa Reli ya SGR kwenye maeneo tofauti ambapo moja ya matukio yaliyotokea ni ukataji wa mita takribani 100 za uzio na majaribio ya kuunganisha nyaya zenye umeme kwenye fensi maalum ya wanyama aina ya tembo hali inayoweza kusababisha hitilafu kwenye uzio huyo”, amesema.
“Uwekaji wa vitu mbalimbali kama matawi ya miti, nyaya za simu, juu ya nyaya za umeme wa kuendeshea treni (catenary system),Kuwepo kwa hitilafu kwenye mfumo wa umeme wa kuendeshea treni kwa vipindi tofauti”. Amesema Kadogosa
Hata hivyo amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa na Shirika ili kukabiliana nazo. “Kuimarisha ulinzi kwa kufanya doria kwenye ushoroba wa Reli kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama, Kuishirikisha jamii kwa kuijengea uwezo kupitia utoaji wa elimu na kusikiliza changamoto zinazowakabili hususan jamii inayoishi kandokando ya reli,” amesema.
“Kuweka kambi katika maeneo mahususi ya reli ili kuwezesha doria za mara kwa mara kwenye maeneo yote muhimu ya uendeshaji na miundombinu ya SGR kama vile Stesheni, Mahandaki, Madaraja, Vituo vya kupozea umeme, Karakana n.k ili kuhakikisha uwepo wa usalama wa abiria na Miundombinu ya Reli.
Vilevile amesema wameendelea kuimarisha uzio na vivuko. “Shirika linaendelea na taratibu za uimarishaji wa vivuko na uzio wa reli kwenye maeneo yalioonekana kuhitaji uboreshaji ikiwemo kuongeza urefu wa uzio wa maalum wa tembo mathalan kati ya Morogoro na Mkata”
“Na shirika linaendelea kutoa mafunzo ya ulinzi na usalama kwa watumishi wote na kuhakikisha taratibu za uendeshaji zinafatwa kadiri ya miongozo mbalimbali ya uendeshaji iliyopitishwa na LATRA”. Amesema Kadogosa.