New Zealand imefanikiwa kutinga katika Kombe la Dunia la FIFA la 2026 baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya New Caledonia kwenye fainali ya ukanda wa Oceanic iliyofanyika Auckland leo asubuhi Mafanikio haya yanaashiria wakati muhimu kwa All Whites, wanapojitayarisha kucheza kwa mara ya tatu Kombe la Dunia, baada ya kushiriki hapo awali mwaka wa 1982 na 2010.
Michuano hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu itafanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, ikiandaliwa kwa pamoja na Marekani, Kanada, na Mexico. Timu ya New Zealand ilionyesha dhamira na ubabe katika muda wote wa mechi, ingawa walijitahidi kupata bao katika kipindi cha kwanza. Wakati muhimu ulikuja baada ya muda wa mapumziko walipopata pigo kwani mchezaji wao nyota, Chris Wood wa Nottingham Forest , alikosekana kwa sababu ya jeraha.
Licha ya kukosekana kwa nyota huyo, All Whites ilipenya safu ya ulinzi ya New Caledonia na kufanikiwa kuuthibiti mchezo kwenye mechi hiyo katika dakika thelathini za mwisho. Beki mkongwe Michael Boxall, mwenye umri wa miaka 36, alitoa mchango wa kukumbukwa kwa kufunga bao lake la kwanza la kimataifa kwa kichwa chenye nguvu katika dakika ya 61.Eli Just, ambaye pia aliingia kama mchezaji wa akiba, alifunga bao la pili dakika ya 81, na kuifungia New Zealand ushindi.
Matumaini ya New Caledonia yanaonekana kuwa hafifu kufuatia kushindwa huku, Timu hiyo itashiriki katika mechi ya mchujo baina ya mabara itakayoshirikisha mataifa sita, ikilenga moja ya nafasi mbili za mwisho zinazopatikana katika Kombe la Dunia. Kupanuka kwa michuano hiyo hadi timu 48 kumeinufaisha New Zealand, ambayo sasa imeorodheshwa ya 89 na FIFA, na kuwaruhusu kufuzu moja kwa moja kwa mara ya kwanza tangu kuhama kwa muundo wa kufuzu. Hili ni badiliko kubwa, haswa tangu kujumuishwa kwa Australia katika Shirikisho la Soka la Asia mnamo 2006. Mbali na mataifa matatu mwenyeji, New Zealand inaungana na Japan, ambayo ilipata kufuzu kwake Alhamisi iliyopita .