Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametaja vipaumbele vya Wizara ya Nishati katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwemo kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji umeme na kufikisha gridi ya Taifa katika Mikoa iliyosalia ya Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara;
Akiwasilisha vipaumbele hivyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Njshati na Madini, leo jijini Dodoma, Dkt. Biteko amesema vipaumbele hivyo vimezingatia mpango wa Taifa wa Nishati wa mwaka 2025 hadi 2030.
“Mhe. Mwenyekiti vipaumbele hivi vimezingatia mpango wa Taifa wa Nishati wa mwaka 2025 – 2030 (National Energy Compact 2025 – 2030) utakaosaidia upatikanaji na uunganishaji wa umeme kwa wananchi, kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme na ushiriki wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya Sekta ya Nishati, ” amesema Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema Serikali imewajengea wazawa uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi ya umeme huku akitolea mfano wa ajira kwenye miradi ya umeme kufikia idadi ya 53,000.
Amesema Dunia inahitaji nishati na mahitaji ya umeme yamekuwa yakiongezeka kwa kasi hivyo Serikali itaendelea kuongeza vyanzo vya kuzalisha umeme ili kukidhi mahitaji ya Watanzania.
Awali, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Nishati, Petro Lyatuu alisema kuwa katika kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika Wizara itaendelea kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Project) pamoja na kufanya matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme;
“Mhe. Mwenyekiti tutandelea na usambazaji wa nishati katika Vitongoji, maeneo ya migodi, kilimo, viwanda na pampu za maji pamoja na vituo vya afya ili kuwezesha shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.” Aliongeza Lyatuu.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia Lyatuu alisema Serikali itaendelea kuhamasisha na kuwezesha watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) na mpango wa Taifa ya Nishati wa mwaka 2025 – 2030 (National Energy Compact 2025 – 2030).
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea na shughuli za utafutaji, uendelezaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia
ikiwemo Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi – Wembere, pamoja na mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi asilia kuwa Kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG Project).
Mradi mwingine ni ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania (East African Crude Oil Pipeline – EACOP).
Vile vile, amesisitiza kuwa Serikali itaendela kuimarisha utendaji wa Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya TANESCO, REA, TPDC, PBPA, EWURA na PURA pamoja na Kampuni Tanzu ili yatoe huduma bora kwa wadau, kuimarisha mapato pamoja na tija na ufanisi katika uendeshaji.
Amesema lengo lingine ni kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme kutoka cha sasa cha asilimia 78.4 hadi kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo ameipongeza Serikali kwa kuja na vipaumbele vitakavyowawezesha watanzania kuwa na nishati ya uhakika.