Na Belinda Joseph, Mbinga – Ruvuma.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mbinga, Mhandisi Mary Kirita ameelezea utekelezaji wa mradi wa uchimbaji visima 900 kwa nchi nzima, ambao unalenga kufanikisha vijiji vitano kila jimbo na Katika Wilaya ya Mbinga Vijijini,
Mradi huo unatekelezwa kwa kutumia vyanzo mbadala vya Mserereko katika vijiji saba, ambavyo ni Barabara, Kilindi, Kindimba Chini, Manzeye, Kihangimauka, Kiwombi, na Kitongoji cha Kipoka kilichopo kijiji cha Kingonsera.
Mhandisi Kirita amesema vijiji vya Barabara na Kilindi ni mojawapo ya vijiji vinavyonufaika na mradi huu, ambapo wananchi zaidi ya 5,500 wanatarajiwa kupata huduma ya maji safi kupitia mradi huu unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 118 unatarajiwa kukamilika kwa mafanikio.
Amefafanua kuwa lengo kuu la mradi huu ni kuhakikisha huduma ya maji inafikia vijiji vyote vinavyokumbwa na uhaba wa huduma hii ambayo itafanikishwa kwa kuchimba visima na kujenga vituo vya maji vinavyojulikana kama point sources, ili kuboresha upatikanaji wa maji safi kwa wananchi.
“Tumeshika hatua za awali kwa kuanza kujenga vituo zaidi ya kimoja na kuweka mtandao wa bomba karibu na maeneo ya makazi, jambo ambalo litaleta urahisi wakati wa upanuzi wa huduma hii katika maeneo mengine,” alisema Mhandisi Kirita.
Mbunge wa Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga, amewataka wakazi wa vijiji vya Barabara na Kilindi kuunganisha huduma ya maji katika kaya zao ili kupunguza changamoto za kupata maji safi, Ameongeza kuwa mabomba yamepita karibu na makazi yao ili kuwasaidia kupunguza gharama za kuingiza maji majumbani.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji Wilaya ya Mbinga mwaka 2025 yalifanyika kwa uzinduzi rasmi wa mradi wa maji wa programu ya visima 900 katika vijiji vya Barabara na Kilindi. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga.
Maadhimisho hayo yalifanyika chini ya kauli mbiu isemayo, “Hifadhi uoto wa asili kwa uhakika wa maji,” ikisisitiza umuhimu wa kuendeleza mazingira kwa ajili ya uhakika wa huduma za maji.