Swaum Katambo – Mpanda.
Taharuki imetanda kwa wakazi wa Mtaa wa Kasimba Kata ya Ilembo Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, baada ya kuonekana mara kwa mara Nyoka aina ya Chatu katika makazi yao huku wakihofia usalama wao.
Wakizungumza viongozi mbalimbali wa Mtaa pamoja na Wananchi wa eneo hilo, kwa pqmoja wameiomba Serikali kupitia Maliasili kuwanusuru na chatu hao ambao wamekuwa wakizuka katika makazi ya watu wakitokea katika mto Kasimba.
Aidha mara baada ya kumuua chatu aliyekuwa akimvizia kuku katika maeneo yao ya makazi, Wananchi hao wamesema Nyoka huyo si wa kwanza huku wakidai uwepo wa chatu wengi ndani ya mto huo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kasimba Benard Nswima ametoa wito kwa wananchi wake kuchukua tahadhali ikiwemo kutofanya shughuli zozote kama kufua nguo pembezoni mwa mto, huku akitoa rai wananchi kujitokeza kwa ajili ya kufanya usafi ili kuondoa nyasi hatarishi pembezoni mwa mto.