Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange amewaelekeza Wauguzi Viongozi wa ngazi zote za afya nchini kuhakikisha wanaimarisha usimamizi wa utoaji wa huduma bora ili wananchi wote wapate huduma bora na kwa usawa
Dkt. Dugange ameyasema hayo leo Machi 27, 2025 wakati akifungua mkutano Mkuu wa Mwaka wa wauguzi viongozi uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa PSSSF Jijini Dodoma wenye kauli mbiu ya inayosema HUDUMA BORA WAJIBU WANGU.
Amefafanua kuwa Serikali ya Awamu ya sita imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya hivyo bila ya kuwepo kwa huduma nzuri na bora kutoka kwa watoa huduma za afya, na hasa Wauguzi, uwekezaji huu hautakua na manufaa.

“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya afya, ununuzi wa vifaa na vifaa tiba, uboreshaji wa mazingira ya kazi, hivyo mapaswa kuwasimamia waliopo chini yenu ili wafanye kazi kwa weledi na uadilifu,” Dkt. Dungange amesisitiza.
Dkt. Dugange amewataka wauguzi wote nchini kuhakikisha wanafanyakazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Miiko ya taaluma ili kuepuka malalamiko yasiyokuwa ya lazima katika eneo la utoaji wa huduma za afya msingi nchini.