Lydia Mollel – Morogoro.
Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wananchi waishio vijijini wanakabiliwa na upungufu wa ulaji wa vyakula vyenye protini, hali inayowaathiri zaidi mama na mtoto,hii ni kwa mujibu wa Mratibu wa Idara ya Mimea na Mazao ya Bustani katika Mradi wa Kilimo, Chakula na Lishe (FoodLAND) kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Susan Nchimbi.
Akizungumza kuhusu matokeo ya tafiti hizo, Prof. Nchimbi alieleza kuwa upungufu huu unaathiri maendeleo ya kiafya na kimwili kwa watoto, pamoja na kudhoofisha kinga ya mwili kwa kina mama.
“Tumegundua kuwa ulajiwa vyakula hususani vyakula vya protini kama mayai na maziwa kwa vijijini ni mdogo karibu asilimia sitini ya walaji tuliowahoji wamekiri kuwa ulaji wa maziwa na mayai nikidogo sana”alisema Nchimbi .
Kwa upande wake, Prof. Dismas Mwaseba, mmoja wa washiriki wa mradi wa FoodLAND, alieleza kuwa mradi huo umekuwa ukiendelea kwa kipindi cha miaka minne na nusu na unahusisha nchi mbalimbali kama Morocco, Tunisia, Ethiopia, Kenya, Uganda na Tanzania.
“Mradi huu unatakribani miaka Minne sasa lengo likiwa ni kuboresha lishe na usalama wa chakula kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo na uboreshaji wa mazao yenye virutubisho vya kutosha,” alifafanua Prof. Mwaseba.
Katika juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo, SUA imeanza mchakato wa kusajili aina mpya za maharage kwa mamlaka husika ili kufanyiwa ukaguzi wa ubora na hatimaye kusambazwa kwa wakulima. Hatua hii inalenga kuongeza uzalishaji wa mazao bora yenye virutubisho kwa ajili ya lishe bora na usalama wa chakula nchini.
Mradi wa FoodLAND unatarajiwa kutoa mapendekezo mahsusi yatakayosaidia kuboresha upatikanaji wa chakula chenye lishe bora, huku jitihada zaidi zikiendelea kufanyika kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo na afya.