Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amesema mwaka wa Fedha wa 2023/2024, Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilipata hasara ya Shilingi bilioni 224 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 102 mwaka uliopita.
CAG amesema hasara hiyo imechangiwa na kupungua kwa mapato ya usafirishaji kutokana na uhaba wa vichwa vya treni na mabehewa pamoja na mvua kubwa iliyosababishwa kufungwa kwa njia kwa miezi minne.
Aidha, Kichere pia amesema “Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lilipata hasara ya Shilingi bilioni 27.78 mwaka wa Fedha wa 2023/2024. Ongezeko hili ni kutoka Shilingi bilioni 4.32 ya hasara kwa mwaka uliopita.”
Hasara hiyo, inachangiwa na ongezeko la gharama baada ya kuhamishiwa Mkongo wa Taifa na Kituo cha Taifa cha Data.