Mafunzo ya siku nne ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama (PSC) la Umoja wa Afrika (AU) yaliyokuwa yakifanyika jijini Arusha yamehitimishwa, ambapo washiriki walipata fursa ya kutembelea hifadhi ya eneo la Ngorongoro.

Akizungumza mara baada ya kuwasili tatika Hifadhi ya eneo la Ngorongoro Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika, Innocent Shiyo ameeleza kuwa baada ya kazi ngumu na ya mafanikio wajumbe wa hao wameona ni vyema kutumia fursa ya kuwepo jijini Arusha kutembelea eneo maarufu duniani la Hifadhi ya eneo la Ngorongoro kwa lengo kujionea vivutio mbalimbali hadimu vinavyopatikana katika hifadhi hiyo.

Balozi Shiyo ameongeza kusema kuwa hatua hiyo ambayo ni muendelezo wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, vilevile inalenga kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania ili kuongeza idadi ya watalii wengi zaidi nchini.

“Tumefarijika sana kuona namna wageni wetu walivyofurahi na kuvutiwa na ukarimu wa Watanzania na mazingira ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro, huku wengi wao wakionesha nia ya kurudi na familia zao ili kupata muda mwingi zaidi wa kujionea mambo mengi mazuri na hadimu yanayopatikana katika hifadhi hii,” alieleza Balozi Shiyo.

Kwa upande wake Kamshina Msaidizi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro Bi. Mariam Chumu Kobelo mbali na kuelezea furaha yake ya kuwapokea wajumbe hao, amewapongeza kwa uamuzi wao wa kutembelea hifadhi hiyo, huku akitoa rai kwao kuwa mabalozi wazuri wa kuelezea mazuri waliyoyaona katika hifadhi hiyo na Tanzania ujumla sehemu mbalimbali duniani.

Mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama la (AU) yalifungwa rasmi Machi 26, 2025 na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika Mhe. Innocent Shiyo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Tanzania yashiriki Mkutano wa Mpango wa Mattei wa Afrika Italia
Maisha: Kila nikienda kwake nakuta zimetumika