Mpango wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Italia na Afrika (The Mattei Plan for Africa and the EU Global Gateway: a common effort with the African Continent) unatarajiwa kuboresha miundombinu ya maendeleo Afrika kwa kuunganisha reli ya Ushoroba wa Lobito kutoka Angola hadi Dar es Salaam (Lobito to Dar Corridor).

Katika mkutano uliofanyika tarehe 27 Machi 2025, jijini Roma Italia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amependekeza Ushoroba wa Lobito upewe jina la Ushoroba wa Lobito – Dar ili kusadifu uwezo wa reli hiyo kuunganisha nchi na nchi kuanzia Bahari ya Atlantiki kwa upande wa Angola hadi Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Ushoroba wa Lobito umeunganishwa na miundombinu ya reli kwa nchi za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Zambia. Mpango wa Mattei utasaidia kuboresha miundombinu ya maendeleo itakayoziunga nchi za Afrika na kurahisisha biashara na uwekezaji bila kusahau umuhimu wa Reli ya TAZARA.

Akizungumza katika mada kuu ya mkutano huo ya uwekezaji katika miundombinu barani Afrika kupitia Ushoroba wa Lobito, Waziri Kombo ameipongeza Italia kwa mpango huu utaoibua fursa nyingi za kimkakati katika sekta za, biashara, uwekezaji, kilimo, madini pamoja na teknolojia kwa kuiunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Ushoroba wa Lobito.

Tanzania ni tajiri wa ardhi yenye rutuba ambayo inaweza kuwanufaisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Kiitaliano katika kilimo haswa kilimo cha kahawa. Uwekezaji utakaosaidia kupunguza changamoto zinazolikumba bara la Ulaya, ikiwemo uhamiaji haramu unaochochewa na ukosefu wa ajira kwa vijana wa Afrika.

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi wa Zambia, Frank Tayali, ameeleza maono ya serikali yao ya kubadilisha Zambia kutoka nchi isiyo na bahari hadi kuwa Taifa kiunganishi ( land linked). Alisisitiza jukumu muhimu la Ushoroba wa Lobito na Reli ya TAZARA katika kuunganisha Zambia na majirani zake nane, kukuza ushirikiano wa kikanda, na kuwezesha biashara chini ya Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 29, 2025
PSC wahitimisha mafunzo kwa ziara ya utalii Hifadhi ya Taifa