Belinda Joseph – Ruvuma.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Ruvuma kuanzia Aprili 2, 2025 hadi Aprili 7, 2025. Ziara hii inalenga kuimarisha chama, kuzungumza na wananchi, na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoa wa Ruvuma, John Foroteo Haule, Balozi Dkt. Nchimbi ataanza ziara yake kwa kupokelewa Wilayani Tunduru, akitokea mkoani Mtwara.

Katika kipindi cha ziara yake, Katibu Mkuu atatembelea Wilaya za Tunduru, Namtumbo, Mbinga, Nyasa, na Songea Mjini, ambapo atafanya mikutano ya hadhara ili kuzungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM na kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Pia, Balozi Dkt. Nchimbi atakagua miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, barabara, kilimo, na maji, huku ziara hii ikiwa ni fursa ya tathmini ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuimarisha ushirikiano kati ya chama, serikali, na wananchi katika kuleta maendeleo endelevu.

Ziara hii inatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo na mshikamano ndani ya chama, na pia kutoa mwanga kwa wananchi kuhusu juhudi zinazofanywa na serikali kuboresha maisha yao. Wananchi wa mkoa wa Ruvuma wanatarajiwa kushiriki kwa wingi katika mikutano ya hadhara, ili kutoa maoni yao na kushiriki katika mchakato wa maendeleo ya taifa.

Tuhuma: Gachagua ni msumbufu, si mkweli - Ruto
Rais Samia ashiriki sala ya Eid kukamilisha mfungo wa Mwezi Mtukufu